1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa kidini wa Iran atoa mwito kuwe na utulivu

Charo Josephat19 Juni 2009

Ayatollah Ali Khamaenei asema Iran ni demokrasia ya kiislamu

https://p.dw.com/p/IUem
Ayatollah Ali Khamenei akiuhutubia umati wa waumini mjini TehranPicha: picture-alliance/ dpa

Kiongozi wa kidini nchini Iran, Ayatollah Ali Khamenei amelihutubia taifa katika matamshi yake ya kwanza hadharani tangu wafuasi wa upinzani walipojitokeza mabarabarani mjini Tehran kushiriki kwenye maandamano makubwa yanayoonekana kuwa changamoto kubwa kwa viongozi wa kidini nchini humo.

Ayatollah Ali Khamenei hii leo ametaka kuwe na utulivu na amani nchini Iran kufuatia siku kadhaa za maandamano ya wafuasi wa upinzani kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais uliompa ushindi rais Mohamoud Ahmadinejad dhidi ya mpinzani wake, Mir Hossein Mousavi.

Akiwahutubia maelfu ya waumini kwenye sala ya Ijumaa katika chuo kikuu cha Tehran, Khamenei amesema jamii ya mapinduzi ya Wairan inahitaji utulivu wa kiakili. Aidha kiongozi huyo amesema ni vigumu kutafuta njia muafaka ya kufuata wakati mtu anapokuwa na ghadhabu wakati alipoanza hotuba yake ambayo kitamaduni hutuwama juu ya maswala ya kidini. Ayatollah Ali Khamenei amesema uchaguzi wa rais uliofanyika hivi majuzi nchini Iran umeudhihirishia ulimwengu kwamba Iran ni taifa lenye demokrasia ya kidini.

"Uchaguzi huu ulikuwa kama mtetemeko wa ardhi kwa maadui zetu. Kwa marafiki zetu, uchaguzi nchini Iran ulikuwa wa kusherehekea. Tulionyesha kukomaa kwa demokrasia ya Kiislamu. Maadui zetu walitaka kuitumia imani yetu katika mfumo wa uchaguzi wetu kuiangusha serikali ya Kiislamu ya Iran.''

Ayatollah Ali Khamenei amesisitiza kwamba maadui wa Iran wanajaribu kufuja imani ya raia kwa taifa lao. Amesema kampeni za uchaguzi zilifanyika kwa uwazi, lakini vyombo vya habari vya kigeni vinavyomilikiwa na wazayuni waovu vililenga kuvuruga uhalali wa uchaguzi huo kwa kuanza kuripoti kwamba udanganyifu ungefanyika hata kabla uchaguzi wenye kufanyika.

Kiongozi huyo wa kidini wa Iran amesisitiza kwamba Wairan wamemchagua kiongozi wanayempenda na kufutilia mbali uwezekano wa kutokoea mizengwe kwenye uchaguzi wa rais. Amethibitisha kwamba rais Ahmadinejad alishinda uchaguzi huo kwa kura milioni 24,5 kati ya kura jumla takriban milioni 40 zilizopigwa. Ayatollah Ali Khamenei pia amesema kwamba maoni ya rais Ahmadinejad yanakaribiana na maoni yake.

Ayatollah Ali Khamenei amesema maandamano ya barabarani hayakubaliki kama njia ya kushinikiza mageuzi nchini Iran na kutaka yakome. Amesema viongozi wa upinzani watakoandaa maandamano watabeba dhamana kwa machafuko yoyote yakayotokea. Amekanusha madai ya kuwepo mpasuko mkubwa miongoni mwa maafisa wa ngazi ya juu wa utawala wa Iran, lakini akakiri kuna tofauti za maoni kati yao.

Ukosoaji

Bildgalerie USA Wahlen McCain Iran 2
John McCain wa chama cha Republican MarekaniPicha: AP

Akizungumza kuhusu hali nchini Iran, senata John McCain wa chama cha Republican nchini Marekani amesema ipo haja ya kutangaza hadharani kwamba uchaguzi wa Iran ulikumbwa na udanganyifu na kusema anawaunga mkono waandamanaji wanaoyapinga matokeo ya uchaguzi huo.

"Tunatakiwa kusema wazi kwamba kumefanyika mizengwe katika uchaguzi wa Iran. Wairan wamenyimwa haki zao na tunawaunga mkono katika juhudi za kuupinga utawala unaowakandamiza."

Wakati huo huo, kamishna wa Umoja wa Mataifa anayehusika na haki za binadamu, Navi Pillay, amesema kukamatwa kwa waandamanaji nchini Iran kunazusha maswali ya kutia wasiwasi. Anasema utawala wa Iran unatakiwa kuhakikisha kesi za waandamanaji waliokamatwa zinafanyika kwa njia ya haki.

Kamishna huyo ameonya kuwa mashambulio dhidi ya wafuasi wa upinzani yanayofanywa na makundi ya wanamgambo yenye mafungamano na serikali huenda yakachochea machafuko na kusababisha hali ya usalama kuendelea kuzorota nchini Iran.