1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani atembelea Mashariki ya kati

Oumilkher Hamidou7 Mei 2009

Matumaini yanayowekewa ziara ya Papa Benedikt wa 16

https://p.dw.com/p/Hlab
Kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguniPicha: picture-alliance/ dpa

Ziara ya kiongozi wa kanisa katoliki duniani,Papa Benedikt wa 16 katika maeneo ya chimbuko la dini ya kikristo,May nane hadi 15 pengine ndio ziara yake muhimu kabisa.Papa Benedikt wa 16 anaanzia Jordan kesho ijumaa.Jumatatu atakwenda Israel .Uhusiano kati ya kanisa katoliki na wayahudi unakumbwa na misuko suko tangu miezi ya hivi karibuni.Kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni alimsamehe askofu mmoja aliyekana mauwaji ya halaiki ya wayahudi-Holocaust.Ziara hii katika ardhi takatifu imejaa vizingiti ndio maana inahitaji busara ya hali ya juu ya kidiplomasia.

Watu wanategemea mengi kabisa kutokana na ziara hii.Wakristo,wayahudi na waislam katika ardhi takatifu wanategemea mengi kutoka kwa kiongozi huyo wa kanisa katoliki ulimwenguni-wanasubiri kutiwa moyo,kupatiwa ufafanuzi na wanategemea kuujua msimamo wake pia.Wote wanataraji ziara ya Papa Benedikt wa 16 itasaidia kuinua hadhi ya wakatoliki bilioni moja na nukta mbili.Upenu si mpana hivyo kwa matamshi na matendo yanayofaa.Ndio maana wataalam wanaiangalia ziara hii kua ni siku nane muhimu kabisa za wadhifa wake kama kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni.Askofu mkuu Salem Al Sayegh ni mkuu wa kanisa katoliki la kiromani nchini Jordan,yeye anasema:

"Hii ni ziara ya kuhiji."

Papa Benedikt wa 16 amesema anafanya ziara ya kuzuru maeneo matakatifu.Inamaanisha:"siji kama mwanasiasa wa kimataifa,siji kama mpatanishi wa ugonvi kati ya waisrael na wapalastina na wala siji kama muokozi katika ugonvi wa nchi za magharibi na dini ya kiislam."Hata hivyo,ziara ya Papa inaangaliwa kama kipimo kidiplomasia kwasababu ardhi hiyo takatifu sio tuu inagombaniwa kisiasa bali hata kwa upande wa imani na maingiliano kati ya waumini wa dini tofauti,inasalia kua eneo tete.

Balozi wa Vatikan nchini Jordan Nuntius Francis-Assisi Chulikat,anajua kwamba makundi ya waislam wenye kufuata itikadi kali mfano wa Udugu wa kiislam wanapinga ziara ya Papa Benedikt wa 16.

"Anakuja kutokana na mwaliko,mwaliko unaotokana na Mfalme mwenyewe.Kwa hivyo yeye ni mgeni rasmi wa Mfalme.Na nnaamini hiyo ndio maana watu wanamkaribisha kwa dhati,licha ya sauti hizo za wanaopinga tunazozisikia kutoka baadhi ya makundi."

Jordan inaangaliwa kama mfano mwema wa kuigizwa katika kuishi pamoja waislam na wakristo katika eneo la mashariki ya kati.Wakristo wa Jordan na nje ya Jordan wanategemea kuona ziara ya kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni ikisaidia kulipatia sura mpya eneo lao.

Shida za kiuchumi na ukosefu wa uungaji mkono ni mambo yaliyopelekea idadi ya wakristo kupungua sana nchini Israel,Palastina na Jordan.Askofu mkuu wa kanisa katoliki la kirumi nchini Jordan Salem Al Sayegh na wakuu wengine wa kanisa katika eneo hilo wanategemea ziara hii ya Papa Benedikt wa 16 itachangia kuzuwia mkondo huo.

Wakristo wa Jordan wanafurahia zaidi ziara ya kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni.Kinyume na mtangulizi wake,Johanna Paulo wa pili,Papa Benedikt wa 16 atasalia siku nne pamoja nao na sio siku moja.

Mwandishi: Dierkes,Theo (WDR)/Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Abdul Rahman