1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa kanisa katoliki awasili Sri Lanka

13 Januari 2015

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ameitolea mwito Sri Lanka kuheshimu haki za binaadamu wakati akianza ziara yake ya mataifa mawili ya Asia leo Jumanne.

https://p.dw.com/p/1EJQf
Papa Francis akiwa na Rais Mithripala Sirisena alipowasili nchini Sri Lanka.
Papa Francis akiwa na Rais Mithripala Sirisena alipowasili nchini Sri Lanka.Picha: Reuters/S. Rellandini

Mwito wa Papa umebeba ujumbe wa amani na maridhiano baada ya vita vilivyodumu kwa miongo kadhaa katika kisiwa hicho

Ziara hiyo ya Papa, inayofanyika siku chache baada ya uchaguzi wa kustajaabisha wa Rais mpya, inajikita katika kuhimiza umoja katika taifa hilo linalopambana kutibu majeraha ya mgogoro wa miaka 37 uliyovipambanisha vikosi vya sereikali na waasi wa kabila la Tamil waliokuwa wanataka kujitenga.

Ziara hiyo ya pili ya Papa Muargentina katika bara la Asia itaihusisha pia Ufilipino, ambayo ni ngome ya ukristo katika kanda hiyo, ambako anatarajiwa kuvutia umati mkubwa zaidi kuwahi kutokea kwa ziara ya kiongozi wa Kanisa Katoliki.

Lakini katika taifa la Sri Lanka lenye waumini wengi wa madhehebu ya Budha, ambalo limeshuhudia ongezeko la vurugu za kidini, Papa Francis atajikita kwenye mchango wa kanisa katika jamii anuwai. "Kazi kubwa ya ujenzi mpya lazima izingatie kuheshimu utu wa watu, haki za binaadamu, na ushirikishwaji kamili wa kila mwanajamii," alisema papa baada ya kuwasili mjini Colombo.

Papa Francis akisalimia umati wa watu alipowasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Bandaranaike
Papa Francis akisalimia umati wa watu alipowasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa BandaranaikePicha: Ishara S. Kodikara/AFP/Getty Images

Kuhusu haki za binadamu

Suala la haki za binaadamu ni nyeti sana nchini Sri Lanka, ambapo imejitenga na jamii ya Kimataifa kwa kukataa kushirikiana na tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa inayochunguza madai ya mauaji ya raia wengi wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe. Papa ambaye alipokelewa na Rais mpya Maithripala Sirisena, alisema mchakato wa uponyaji pia unahitaji kuhusisha ufuatiliaji wa ukweli.

Sirisena ambaye aliingia madarakani siku chache zilizopita, ameahidi kuunda tume huru ya uchunguzi katika madai ya ukiukaji wa haki za binadaamu wakati wa vita chini ya mtangulizi wake Mahinda Rajapaksa. Waziri wake mkuu mpya Ranil Wickremesinghe alisema kabla ya uchaguzi kuwa serikali yake itaunda tume ya ukweli na maridhiano, sawa na ile ya Afrika Kusini.

Ni karibu asilimia 6 tu ya raia milioni 20 wa Sri Lanka ndiyo waumini wa Kikatoliki, lakini dini hiyo inatazamwa kama nguzo muhimu ya maelewano kwa sababu inahusisha watu kutoka makabila mawili , Sinhale ndilo kubwa zaidi, na lile la wachache la Tamil.

Kesho Jumatano, ambayo imetangazwa kuwa siku ya mapumziko, papa ataendesha misa kuu mjini Colombo, ambayo inatarajiwa kuhudhuriwa na karibu watu milioni moja, ambapo pia anatarajiwa kumtangaza mtakatifu Mmishonari wa Sri Lanka wa karne ya 17, kabla ya kutembelea kanisa lililoko katika msitu ambako ulianzia mgogoro wa kikabila uliyowauwa watu karibu laki moja.

Mnamo siku ya Alhamisi, kiongozi huyo mkuu wa Kanisa Katoliki duniani ataelekea Ufilipino

Mwandishi: Zuhura Hussein/AFP

Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman