1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa chama kikuu cha Upinzani nchini Zimbabwe cha MDC, Morgan Tsvangirai na harakati za Kisiasa.

Scholastica Mazula28 Machi 2008

Pamoja na Misukosuko ya mashitaka ya uhaini na kupigwa vibaya na Vikosi vya Usalama na kugawanyika kwa Chama chake, Morgan Tsvangira ameendelea kuonyesha ushupavu wake katika siasa.

https://p.dw.com/p/DWic
Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai.Picha: AP

Kiongozi huyo wa chama kikuu cha Upinzani nchini Zimbabwe cha Movement for Democratic Change-MDC, Morgan Tsvangirai ameendelea kumkalia kooni Mugabe tangu mwaka 1990.

Morgani Tsvangirai ambaye anaamini kuwa ni udanganyifu wa kura tu, utakaofanywa na Rais Robert Mugabe wa nchi hiyo, ndiyo utakaomfanya ashindwe katika uchaguzi wa kesho.

Mbali na kwamba Rais Mugabe ameapa kwamba kamwe Morgan Tsvangirai hawezi kushinda ili hali yeye yungali hai, Tayari Tsvangirai ameshamuonya rais huyo kwamba endapo atajaribu kuiba kura katika uchaguzi wa kesho basi hali ya mambo itazidi kuwa mbaya zaidi nchini humo.

Kiongozi huyo wa Chama Kikuu cha Upinzani nchini humo cha MDC, amekuwa mpinzani Mkuu wa Rais Robert Mugabe tangu miaka ya 1990.

Katika kampeni zake amekuwa akisisitiza kwamba alikuwa mshindi wa haki katika uchaguzi wa mwaka 2002 lakini kutokana na mbinu za mpinzani wake ambaye ni rais Mugabe za kuiba kura alionekana ameshindwa.

Pamoja na misukosuko yote aliyoipitia anasema ni lazima chama chake kishinde katika uchaguzi wa kesho.

Kutokana na kuvunjwa moyo na matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2002, Tsvangirai alionekana kujivuta kujitumbukiza katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa mwaka huu lakini hatimaye mwezi Februari aliamua kujitosa kikamilifu katika kinyang'anyiro hicho.

Uchumi wa Zimbabwe umekuwa ukidhoofika na ughali wa maisha hivi sasa umezidi asilimia laki moja , wakati huohuo zaidi ya asilimia themanini ya raia wake hawana ajira.

Lakini matarajio ya Morgan Tsvangirai yameingia dosari kutokana na mgawanyiko katika chama chake cha MDC, uliosababishwa na mvutano juu ya ikiwa chama hicho kigombee nafasi ya juu katika uchaguzi wa mwaka 2005, uchaguzi ambao ulikifanya chama hicho kushindwa vibaya kwa karibu nusu ya wabunge katika chama hicho walishindwa.

Hivi sasa Morgan Tsvangirai anapambana na changamoto nyingine kutoka kwa Waziri wa fedha wa zamani wa Zimbabwe Simba Makoni ambaye Tsvangirai amekiri kuwa ni mzalendo shujaa lakini siyo kiini cha mabadiliko.

Kwa mara ya kwanza Morgan Tsvangirai alinza kupambana na Mugabe wakati akiwa Katibu Mkuu wa baraza la vyama vya wafanyakazi nchini Zimbabwe, ambapo aliongoza migomo mbalimbali ya kupinga kiwango cha juu cha ushuru katika miaka ya 1997 na 1998.Hata hivyyo dai lake hilo halikukubaliwa na wapinzani wake.

Mwezi Septemba mwaka 1999, alianzisha chama cha Movement for Democratic Change-MDC, na kilishinda karibu nusu ya viti vya wabungee katika uchaguzi uliofuatia wa mwaka 2002, mbali na kwamba kampeni hizo ziligubikwa na vurugu ambazo zilisababisha kuuawa kwa wafuasi wake thelathini.

Morgan Tsvangirai alisimama na kuanza kazi rasmi ya kisiasa mwaka 2001 alipostakiwa kuwa anapanga njama za kumuua Mugabe katika kesi iliyotolewa ushahidi na aliyekuwa jasusi wa Serikali ya Israeli.Hata hivyo alishinda kesi hiyo.

Alishitakiwa kwa kesi nyingine za uhaini na kupigwa lakini siku zote amekuwa akisema kwamba ni kweli walimfanyia vitendo vya kinyama, lakini hawawezi kumuondolea nia yake na ataendelea kuwa asikari shupavu hadi hapo Zimbabwe itakapokuwa huru.

Morgan Tsvangirai alizawaliwa mwaka 1952 huko Gutu Zimbabwe ni mtoto wa kwanza kati ya watoto nane na baba yake alikuwa mwashi.

Baada ya masomo yake alitumia muda wake wa miaka kumi akiwa katika machimbo ya madini ya Nikeli kkwenye jimbo la kati la Mashonaland na baadaye akawa msimamizi kabla hajajiingiza katika masuala ya Kisiasa.