1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kinyang'anyiro cha madaraka nchini Misri

11 Julai 2012

Mvutano kati ya jeshi na chama cha Udugu wa kiislamu umezidi makali baada ya korti kuu ya katiba kuamua kubatilisha kanuni ya rais Mohammed Mursi aliyeamuru bunge likutane upya.

https://p.dw.com/p/15VFt
Rais Mursi (wa tatu kutoka kushoto) na mkuu wa baraza la kijeshi,Hussein Tantawi(wa pili kutoka kulia) wakihudhuria sherehe za kukabidhiwa shahada maafisa wa jeshi la wanaangaPicha: picture-alliance/dpa

"Korti kuu ya katiba imeamua kusitisha kanuni ya rais" mkuu wa korti hiyo, jaji Maher el Beheiry amesema na kuamuru amri ya awali ya korti hiyo iheshimiwe.

Uamuzi huo umepitishwa katika wakati ambapo bunge lilikuwa linakutana. Wabunge wa vyama vya kiislamu ikiwa ni pamoja na wale wa Udugu wa kiislamu,chama cha Haki, na wabunge wa Salafiya, ndio waliohudhuria kikao hicho kifupi kilichosusiwa lakini na wabunge kadhaa wa mrengo wa shoto na pia wale wa kiliberali.

"Tunakutana kutathmini uamuzi uliopitishwa na korti kuu ya katiba," alisema spika wa bunge hilo, Saad al Katatni.

"Nataka kusisitiza hatuuendei kinyume uamuzi uliopitishwa, tunatafuta njia za namna ya kuanza kufanya kazi uamuzi wa korti hiyo inayoheshimiwa. Hakuna la ziada katika ratiba ya leo, amesisitiza spika huyo wa bunge na kuongeza kuwa wameomba kesi hiyo isikilizwe upya na mahakama maalumu.

Ägypten Parlamentssitzung
Kikao cha bunge la MisriPicha: AP

Mamia ya watu wanaendelea kukusanyika katika uwanja wa Tahrir mjini Cairo, wakiimba nyimbo kumsifu rais Mohammed Mursi na kuwalaani wanajeshi.

Uamuzi wa Mursi ulisifiwa na wale wanaopendelea kuwaona wanajeshi wakirejea kambini, lakini ulikosolewa na wale wanaohofia wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kiislamu wasije wakahodhi madaraka yote nchini humo.

Wakati huo huo, rais mpya wa Misri Mohammed Mursi anapanga kufanya ziara yake ya kwanza nchi za nje kwa kuitembelea Saud Arabia hii leo.

Ägypten Mursi Westerwelle JANUAR 2012
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido Westerwelle akizungumza na rais Mursi mjini CairoPicha: picture-alliance/dpa

Jana rais Mursi alikuwa na mazungumzo na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle. Mwishoni mwa mazungumzo hayo, waziri Westerwelle alisema:"Rais amenihakikishia kwa mara nyengine tena, habishi uamuzi wa korti kuu wa kulivunja bunge, ina maana kwa hivyo kutafuta njia za kuitishwa haraka iwezekanavyo uchaguzi wa bunge, naiwe jumla au kwa sehemu."

Ufumbuzi wa mzozo kati ya rais na wafuasi wa Udugu wa kiislamu na wanajeshi uko mbali kupatikana.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Hillary Clinton, anatazamiwa kufika ziarani mjini Cairo Jumamosi ijayo. Anapanga pia kuzitolea mwito pande zote zinazohusika zijadiliane kwa dhati.

"Tunahimiza majadiliano yaendelezwe ili wananchi wa Misri wapate kile walichokipigania na kukipigia kura," amesema waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Marekani.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters

Mhariri:Josephat Charo