1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KINSHASA:Kongo na Uganda kujadilia mzozo wa mpaka

15 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBZ0

Nchi za Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo zinakubali kujadilia mzozo wa mpaka ambapo majeshi ya Kongo yalimpiga risasi hadi kufa mfanyikazi mmoja wa kiwanda cha mafuta aliye na asili ya Uingereza.

Kongo kwa upande wake ilikuwa inalipiza kisasi baada ya majeshi ya usalama ya kampuni ya mafuta ya Heritage Oil kuchimba mafuta kinyume na sheria kwenye eneo lake la Ziwa Albert.Ziwa Albert linatapakaa kwenye mataifa yote mawili ya Kongo na Uganda.

Kwa mujibu wa waziri wa mambo ya nje wa Uganda Sam Kutesa mataifa hayo jirani yanapanga kukutana mwishoni mwa mwezi huu ili kujadilia suala hilo.Uganda inasisitiza kuwa haitashambulia eneo la Kongo la mpakani ila kujilinda.

Kongo kwa upande wake inapanga kufanya mkutano mwezi ujao mjini Kampala utakaohudhuriwa na wawakilishi wa Rwanda,Burundi na Uganda.Antipas Mbusa Nyamwisi ni waziri wa wa Mambo ya Nje wa Kongo

''Wakongomani wanashika doria kwa saa 24 na wanajeshi wa Uganda walioko ngambo ya pili wanaonekana kujiandaa kwa shambulio ambalo hatutaki.Hata hivyo majeshi hayo yanawazuia wavuvi wa Uganda kufika kwenye kisiwa hicho.Cha msingi ni kuwa endapo watatushambulia tena tutalazimika kulipiza kisasi.''

Ziwa Albert lililo kwenye Bonde la Ufa ni eneo linaloaminika kuwa na mafuta.Kampuni ya mafuta ya Heritage inachimba mafuta kwenye eneo la Uganda la Ziwa hilo huku serikali ya Kongo ikishikilia kuwa haina ruhusa ya kutafuta mafuta kwenye eneo lake la Ziwa hilo.