1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KINSHASA : Waasi washambulia vikosi vya serikali

25 Novemba 2006
https://p.dw.com/p/CCpV

Wapiganaji wafuasi wa generali alieasi wameshambulia maeneo ya wanajeshi wa serikali mashariki mwa Congo kwa kutumia silaha ndogo na silaha nzito.

Shambulio hilo kufuatia utulivu wa kiasi fulani uliodumu kwa miezi kadhaa kwenye eneo la vurugu la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo limekuja wakati kukiwa na hali ya mvutano katika mji mkuu wa Kinshasa ambapo wafuasi wa kiongozi wa zamani wa waasi Jean Piere Bemba wanapinga ushindi wa Rais Joseph Kabila katika marudio ya uchaguzi wa rais mwezi uliopita.

Waziri wa mambo ya ndani wa Congo Denis Kalume ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters leo hii kwamba sehemu zao za kijeshi huko Sake zimekuwa zikishambuliwa na generali muasi Nkunda tokea asubuhi na mapema na kwamba vikosi vyao vilioko huko vimekuwa vikijibu mapigo.

Duru za Umoja wa Mataifa zimethibitisha kutokea kwa shambulio hilo leo ashubuhi huko Sake ambalo ni eneo la mstari wa mbele wa mapambano kati ya waasi na wanajeshi wa serikali kilomita 20 magharibi mwa mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini karibu na mpaka na Rwanda.