1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KINSHASA : Congo yakataa operesheni za kijeshi

20 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CC90

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo hapo jana imefuta uwezekano wa operesheni za kijeshi na mataifa jirani ndani ya ardhi yake kuwasaka waasi katika eneo la Maziwa Makuu lililokumbwa na mfarakano.

Waziri wa mambo ya nje Antipas Mbusa Nyamwisi amewaambia waandishi wa habari kwamba wakuu wa kijeshi wa Jamhuri ya Kidemokarsi ya Congo,Uganda,Rwanda na Burundi wamepitisha mkakati wa kijeshi wa pamoja mjini Bujumbura kusaka makundi ya watu wenye silaha yalioko mashariki mwa nchi hiyo.

Hata hivyo amesema ni jambo lisilokubalika kisiasa kwamba vikosi vya kigeni vinaweza kuendesha shughuli zake katika ardhi ya Congo.

Eneo la nchi za Maziwa Makuu limekumbwa na umwagaji damu tokea mapema katika miaka ya 1990 kwa kuanzia na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi hapo mwaka 1993, mauaji ya kimbari ya Rwanda hapo mwaka 1994 na vita vya kanda vilivyorindima katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kati ya mwaka 1998 hadi mwaka 2003.