Kimbunga Nate chashambulia eneo la Mississippi
8 Oktoba 2017Wakati kimbunga hicho kinachokwenda kwa kasi kubwa kikielekea katika pwani ya Mississippi, ambako kinatarajiwa kushambulia eneo hilo na kutishia kusababisha mvua kubwa na mafuriko ambayo yataharibu nyumba na biashara.
Kimbunga Nate kilitarajiwa kupita mashariki mwa New Orleans, kikiepuka kuushambulia mji huo kwa upepo wake mkali . Na kasi yake kubwa ilipunguza uwezekano wa mvua kunyesha kwa muda mrefu ambazo zingeharibu mfumo dhaifu wa kusukuma maji taka.
Pamoja na hayo, mji huo ambao ni maarufu kwa pati za usiku kucha uliwekwa katika amri ya kutotembea usiku, kuanzia saa moja jioni na mitaa haikuwa imejaa watu kama ilivyo kawaida yake katika usiku wa Jumamosi.
Miji katika pwani ya Mississippi kama Gulfport na Biloxi ilikuwa katika tahadhari ya juu. Baadhi ya hoteli zilizoko katika eneo la ufukwe na kasino watu waliondolewa. Kimbunga Nate kilidhoofika kidogo na kilikuwa katika kiwango cha kimbunga namba moja kikiwa na upepo unaokwenda kwa kasi ya kilometa 85 kwa saa wakati kiingia katika eneo hilo ambalo linaishi watu wachache la Plaquemines.
Watabiri wa hali ya hewa walisema inawezekana kwamba kimbunga hicho kikaimarisha nguvu zake na kuwa katika kiwango cha kimbunga namba mbili , lakini inaonekana uwezekano huo kuwa mdogo wakati usiku ukiingia.
Hali ya hatari yatangazwa
Kasi ya kimbunga hicho ilitishia jamii inayoishi mabondeni kusini mashariki mwa Louisiana , mashariki mwa kijiji cha wavuvi cha Alabama cha Bayou la Batre.
"Iwapo kutakuwa na mafuriko tena, haya ndio yatakuwa," amesema Larry Bertron wakati yeye na mke wake wakijitayarisha kuondoka nyumbani kwao katika jamii ya Braithwaite ya eneo la parishi ya Plaquemines ambayo huathirika mara kwa mara na mafuriko.
Magavaan mjini Louisiana , Mississippi na Alabama wametangaza hali ya hatari. Majimbo hayo matatu hayakupata madhara makubwa katika kipindi hiki cha vimbunga.
Maafisa wamewaokoa watu watano kutoka katika maboti mawili katika wakati wa mawimbi makubwa kabla ya kimbunga hicho kuwasili. Boti moja ilipoteza ingini yake katika ziwa Pontchartrain na watu wawili waliokuwamo katika boti hiyo waliokolewa.
Gavana wa Louisiana John Bel Edwards amewahimiza wakaazi kufanya matayarisho ya mwisho haraka na kusisitiza kwamba kimbunga Nate kitaleta uwezekano wa upepo mkali ambao unaweza kusababisha mawimbi makubwa yanayofikia futi 11 katika baadhi ya maeneo ya pwani.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Zainab Aziz