1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kimbunga Gustav chasababisha mvua kubwa Louisiana

Charo, Josephat1 Septemba 2008

Rais Bush aenda Texas, McCain abadili ratiba ya mkutano wa chama cha Republican

https://p.dw.com/p/F8Sl
Mawingu ya kimbunga Gustav yakitanda juu ya anga ya mji wa New OrleansPicha: AP

Huku kimbunga Gustav kikihatarisha maisha ya Wamarekani wengi, rais George W Bush anataka kulidhihirishia taifa kwamba serikali yake imejifunza mengi kutokana na uharibifu uliosababishwa na kimbunga Katrina miaka mitatu iliyopita. Chama cha Republican kimeahirisha baadhi ya ratiba muhimu kwenye mkutano wake mkuu unaolenga kumteua rasmi John McCain kugombea urais wa Marekani katika uchaguzi wa mwezi Novemba mwaka huu.

Mvua kubwa iliyosababishwa na kimbunga Gustav imeanza kunyesha katika mwambao wa ghuba la Mexico mapema leo baada ya watu takriban milioni mbili kulazimika kukikimbia kimbunga hicho. Mamia ya wanajeshi wamepelekwa katika mji wa New Orleans baada ya kile kinacholelezwa kuwa harakati kubwa ya kuwahamaisha watu katika historia ya Marekani. Watu watatu waliokuwa wagonjwa mahututi wanaripotiwa kufariki dunia wakati walipokuwa wakihamishwa kutoka eneo hilo hatari.

Watu yapata milioni mbili wameikimbia pwani ya Louisiana na wengine zaidi ya milioni 11 katika majimbo mengine matano ya Marekani wanajiandaa kukabiliana na kimbunga Gustav. Kampuni za mafuta zimefunga shughuli zake zote za kuchimba mafuta katika ghuba ya Mexico, aneo linalotoa asilimia 25 ya mafuta ya Marekani na asilimia 15 ya gesi yake. Bei za mafuta zimepanda hii leo kutokana na kimbunga Gustav na kufikia dola 116.01 kwa kila pipa.

Kimbunga Gustav kimeathiri ratiba ya mkutano mkuu wa chama cha Republican unaoanza leo huko St Pauli, Minneapolis unaolenga kumteua rasmi John McCaina kugombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi wa Novemba baadaye mwaka huu.

Akizungumza kuhusu uamuzi wa kuifanyia mabadiliko ratiba ya mkutano wa chama cha Repulican, mgombea urais wa chama hicho John McCain amesema, ´´Halitakuwa jambo la busara kuendelea na mkutano wetu wa chama, kama tulivyokuwa tumepanga, huku changamoto kubwa na hatari ikiwa imejitokeza kwa mfano wa janga asili.´´

Rais Bush kukosa mkutano wa chama

Rais George W Bush amesema hatohudhuria mkutano wa chama chake cha Repulican huko Minneapolis hii leo. Badala yake anakwenda Texas, jimbo ambalo limechaguliwa kuwa makaazi na uwanja wa operesheni ya kutoa huduma za dharura kwa wakaazi wa pwani ya ghuba ya Mexico waliokikimbia kimbunga Gustav.

´´ Kimbunga hiki ni hatari. Sitakwenda Minnesota kuhudhuria mkutano mkuu wa chama cha Republican. Kesho nitakwenda Texas kutembelea kituo cha kutoa huduma za dharura na kushuhudia harakati zinazofanywa na maafisa wa serikali. Sitakwenda Lousiana hapo kesho kwa sababu sitaki ziara yangu iwatatize kwa njia yoyote ila, wafanyakazi wa kutoa huduma za dharura.´´

Rais George W Bush ameonya kwamba mafuriko makubwa huenda yakatokea na amewataka raia katika eneo hilo wafuate maagizo na maelekezo ya maafisa wa serikali kuu na ya jimbo na wasijiweke katika hali ya hatari wala kuwalazimisha waokoaji kuchukua hatua zitakazoyatarisha maisha yao.

Rais Bush amesema atawahimiza watu nchini kote wawasaidie majirani wao wenye mahitaji, kuchanga pesa kwa mashirika ya misaada kama shirika la msalaba mwekundu na watumie muda wao kuwasaidia wenye mahitaji na kuwaomboea wale ambao pengine watakuwa wakiteseka kutokana na athari za kimbunga Gustav.

Watabiri wa hali ya hewa wanasema kimbunga Gustav chenye upepo wa kasi ya kilomita 115 kwa saa, kinabakia katika daraja ya tatu na kinatarajiwa kusababisha hasara ya jumla ya dola bilioni 38 za kimarekani katika majimbo ya Louisiana, Mississipi na Alabama.