1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kim Jong Il afariki dunia

Mohammed Khelef19 Desemba 2011

Televisheni ya serikali ya Korea ya Kaskazini imetangaza kuwa kiongozi wa nchi hiyo, Kim Jung Il, amefariki dunia akiwa kwenye treni katika ziara ya kikazi, baada ya kuzidiwa na shinikizo la damu la ghafla.

https://p.dw.com/p/13VMd
Wanajeshi wa Korea Kusini wakiangalia taarifa ya kifo cha Kim Jon Il kwenye televisheni.
Wanajeshi wa Korea Kusini wakiangalia taarifa ya kifo cha Kim Jon Il kwenye televisheni.Picha: dapd

China imesema ina majonzi sana kwa kifo cha Kim Jon Il na imeungana na raia wa Korea Kaskazini kuomboleza kifo cha swahiba wake mkubwa. Rais Barack Obama wa Marekani amempigia simu mwenzake wa Korea Kusini, Lee Myung-Bak, usiku wa manane, kutathmini kifo hicho. Usalama umeimarishwa mpakani mwa Korea hizo mbili. Huko Japan, masoko ya hisa yameanguka kwa zaidi ya asilimia 1.26 kufuatia taarifa za kifo hiki.

Hivi ndivyo ulimwengu ulivyokipokea kifo cha kiongozi huyu, na hivyo ndivyo uzito wa "Kiongozi Mpendwa", kama alivyokuwa akijuilikana nchini mwake, unavyoonekana. Kim Jong Il aliingia madarakani mwaka 1994 baada ya kifo cha ghafla cha baba yake, Kim Il Sung, ambaye alikuwa ameliongoza taifa hilo tangu mwaka 1948.

Miongoni mwa mafanikio ya mwanzo ya Kim Jong Il, yalikuwa ni kuivaa tabia na haiba ya baba yake, na hivyo kujijengea mvuto ambao kabla hakuwa nao. Wengi wanasema, kuwepo kwa Jong Il madarakani kulikuwa sawa na kuwapo kwa Il Sung.

Kielimu, Kim Jong Il alisoma kwanza nchini China kabla ya kujiunga na chuo kikuu cha Kim Il Sung mjini Pyongyang alikosomea siasa na uchumi. Aliingia rasmi kwenye siasa mwaka 1964, kwa kujiunga na chama pekee cha siasa, chama tawala cha Wafanyakazi cha Korea, ambako alipanda vyeo haraka haraka.

Akiwa na miaka 31 tu hapo mwaka 1973, aliteuliwa kuwa katibu mkuu wa mipango na propaganda, na mwaka mmoja baadaye akatangazwa rasmi kuwa mrithi wa baba yake. Mwaka 1980 aliingia kwenye Kamati ya Ulinzi, ambacho ndicho chombo cha juu kabisa kiutawala. Mwaka 1991 akatangazwa kuwa kamanda mkuu wa majeshi.

Waombolezaji nchini Korea Kaskazini.
Waombolezaji nchini Korea Kaskazini.Picha: dapd

Si mengi yanayojulikana na ulimwengu wa nje kuhusu kiongozi huyo. Vyombo vya habari vya Magharibi vinajaribu kumuelezea kama mwanamme anayevaa suti za Mao na miwani meusi, anayependa wanawake, ulevi, vyakula na magari ya kifahari, lakini asiye na ufahamu sana wa mambo ya dunia. Maisha yake binafsi, yakiwemo mahusiano yake na maisha ya watoto wake wanne, yalikuwa ni mwiko kuzungumzwa kwenye vyombo vya habari vya serikali.

Hata hivyo, rais wa zamani wa Korea ya Kusini, Kim Dae Jong, anamuelezea kama mtu mwenye akili inayofanya kazi haraka na ambaye anajua kila kitu kinachoendelea ulimwenguni. Hii ilikuwa ni baada ya viongozi hao wawili kukutana katika mkutano wa nadra baina ya viongozi wakuu wa mataifa hayo mwaka 2000.

Kwa raia milioni 23 wa Korea Kaskazini, Kim Jong Il alifahamika kama mwanamapinduzi, mtu mwenye akili katika masuala ya fasihi, sanaa na mikakati ya kijeshi. Picha zake na za baba yake, aliyepewa vyeo vya Kiongozi Mkuu na Rais wa Kudumu, Kim Il Sung, zinaning'inia karibuni katika kila jengo na nyumba.

Uvumi kuhusiana na afya yake ulianza kusambaa mwaka 2008, baada ya kushindwa kuhudhuria sherehe za miaka 60 ya uhuru wa nchi yake. Haraka Korea Kaskazini ikakanusha taarifa za kijasusi za Korea Kusini zilizosema kuwa kiongozi huyo alikuwa anaugua shinikizo la damu na kwamba alipata ugonjwa wa kiharusi.

Msingi hasa wa sera zake binafsi haukufahamika hadi anafariki dunia. Hata hivyo, jambo moja lilikuwa wazi: Mara kadhaa Kim Jong Il aliitunishia kifua Marekani, na kwa mujibu wa mantiki ya Korea ya Kaskazini, kuwa na silaha za nyuklia ndiyo njia pekee ya kuepuka kushambuliwa na Marekani. Licha ya umasikini na ukame ulioidumaza kabisa nchi yake, Kim Jung Il atakumbukwa kama kiongozi aliyeliongoza taifa lenye jeshi kubwa kabisa duniani.

Kama yeye alivyorithi madaraka kutoka kwa baba yake, naye sasa anarithiwa na mtoto wake wa tatu wa kiume, Kim Jong-Un, ambaye ndiyo kwanza hajafikia umri miaka 30.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters/DPA
Mhariri: Saumu Mwasimba