1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kikosi cha Afrika Kusini chawasili Afrika ya Kati

7 Januari 2013

Afrika Kusini imetuma wanjeshi 400 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, kusaidia vikosi vya nchi hiyo chini ya kile kinachotajwa kuwa kutimiza majukumu ya kimataifa. Nao waasi wa Seleka wameuteka mji mwingine nchini humo.

https://p.dw.com/p/17F3L
Wanajeshi kutoka nchi za kanda waliofika kuisaidia serikali ya rais Francois Bozize
Wanajeshi kutoka nchi za kanda waliofika kuisaidia serikali ya rais Francois BozizePicha: SIA KAMBOU/AFP/Getty Images

Kuwasili kwa wanajeshi hao wa Afrika Kusini kumethibitishwa na ofisi ya rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Tangazo lililotolewa na ofisi hiyo limesema kwamba kutumwa kwa wanajeshi hao kumeamriwa na rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma.

Tangazo hilo liliongeza kwamba wanajeshi hao wa Afrika Kusini wataliongezea uwezo jeshi la Jamhuri ya Afrika ya Kati, na kuisaidia nchi hiyo katika mpango wake wa kuyapokonya silaha makundi ya wanamgambo na kuwarejesha katika maisha ya kiraia.

Wizara ya ulinzi ya Afrika Kusini pia imetoa tamko kuhusu kutuma wanajeshi wake. ''Kwa kuzingatia hali ya kiusalama katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jeshi la Ulinzi wa Taifa la Afrika Kusini limetuma msaada na timu ya ulinzi'', lilisema tangazo la wizara hiyo.

Waasi wauteka mji mwingine

Wanamgambo wa Seleka wamekuwa wakisonga mbele kuelekea mji mkuu wa Afrika ya Kati, Bangui, tangu walipoanza mashambulizi mwezi Desemba. Mashambulizi yao yamezifanya Ufaransa, Marekani na pia Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika ya Kati kutuma wanajeshi katika nchi hiyo.

Waasi wa Seleka wamekuwa wakisonga mbele kuusogelea mji mkuu, Bangui.
Waasi wa Seleka wamekuwa wakisonga mbele kuusogelea mji mkuu, Bangui.Picha: SIA KAMBOU/AFP/Getty Images

Jumamosi waasi wa Seleka waliukamata mji wa Alindao ulioko umbali wa KM 500 mashariki mwa mji mkuu Bangui, bila kupata upinzani wowote. Waasi hao walikata nyaya zote za simu katika mji huo.

Kwa sasa waasi sasa wameiteka miji 11. Awali walikuwa wamesema kuwa wameacha kusonga mbele, wakisubiri mazungumzo na serikali ya rais Bozize. Kukamatwa kwa mji wa Alindao kumezusha mashaka juu ya uwezekano wa kufanyika kwa mazungumzo hayo, ambayo yalipangwa kufanyika kesho Jumanne mjini Libreville nchini Gabon.

Jumuiya ya kimataifa yatoa wito wa mapatano

Marekani ilikuwa imezitaka pande zinazohasimiana kuyatumia mazungumzo hayo kumaliza tofauti zao kwa amani, lakini waasi wa Seleka walitangaza Ijumaa kwamba hawajaarifiwa kuhusu mazungumzo hayo.

Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Francois Bozize amekataa wito wa waasi kuachia madaraka
Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Francois Bozize amekataa wito wa waasi kuachia madarakaPicha: dapd

Msemaji wa waasi hao Eric Massi aliliambia shirika la habari la AFP kwamba hawana habari yoyote kuhusu maandalizi ya mazungumzo hayo, kauli ambayo ilikinzana na taarifa ya Jumuiya ya kiuchumi ya Afrika ya Kati, iliyosema kwamba waasi wameafiki kushiriki katika mazungumzo hayo katika mji mkuu wa Gabon, Libreville.

Waasi wa Seleka wanamshutumu rais Francois Bozize kuvunja mkataba wa amani wa hapo awali, na kumtaka aachie madaraka. Hata hivyo rais huyo amesema haondoki kabla ya kumaliza muhula wake mwaka 2016.

Umoja wa Mataifa unakadiria kwamba wananchi zaidi ya 300,000 ambao ni asilimia 7 ya wakazi wote milioni 4.6 wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, wanaishi katika maeneo yenye mizozo. Makadirio hayo pia yanaonyesha kuwa wakazi 700,000 wa mji mkuu Bangui, wataathirika ikiwa mapigano yataendelea baina ya waasi na serikali.

Mwandishi: Daniel Gakuba/DPE/AFP/AP

Mhariri:Hamidou Oummilkheir