1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kikao cha mwaka cha Umoja wa mataifa chafunguliwa

Nijimbere, Gregoire23 Septemba 2008

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon amekifungua kikao cha mwaka cha Umoja wa mataifa mjini New York Marekani, akitoa wito kwa viongozi duniani kujenga kile amekitaja ´´uongozi wa dunia´´

https://p.dw.com/p/FNg8
Ban Ki-Moon, Katibu mkuu wa Umoja wa mataifaPicha: AP

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao hicho cha Umoja wa mataifa, Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa amewatolea wito viongozi wa dunia wasizingatie maslahi ya mataifa yao tu, bali wazingatie nchi zote kwa jumla. Dalili zaonyesha hali sio hivyo ilivyo kwa sasa.Ban Ki-Moon amesema hali hiyo inatia wasi wasi:

´´Mataifa hayawezi kuendelea kuyalinda maslahi yao au kuendeleza maisha mema ya watu wao bila ushirikiano na ulimwengu. Nina wasi wasi kwamba leo kuna hatari ya kutoona ukweli huo wa mambo. Ninaona kuna hatari kubwa nchi kuangalia ndani yake badala ya kuangalia mbele.

Ninaona kuna hatari ya kurudisha nyuma maendeleo tumekwishafikia hususan masuala ya maendeleo na kugawana sawa matunda ya ukuaji uchumi duniani.´´


Ban Ki-Moon ameyasema hayo akitoa orodha ya changamoto chungu nzima zinazoikabili dunia wakati huu. Miongoni mwa changamoto hizo, ni pamoja na migogoro ya fedha, nishati, chakula, mkwamo wa mazungumzo juu ya Mkataba wa biashara duniani na ongezeko la joto duniani. Ban Ki-Moon amesema dunia sasa inahitaji viongozi wanaoweza kuuelekeza ulimwengu mzima katika juhudi za kukabiliana na changamoto hizo. Kinachohitajika zaidi ni ushirikiano kuliko mvutano, ameongeza kusema Ban Ki-Moon. Maada ya kutekeleza mipango ya maendeleo ya Millenia ndio itapewa kipau mbele katika kikao hicho cha siku tano, amesema Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa.

Rais wa Marekani George W. Bush, ni rais wa kwanza ambae amekihotubia kikao hicho cha Umoja wa mataifa, ikiwa ndio hotuba yake ya mwisho kama rais wa Marekani ikiwa imesalia miezi minne tu kabla ya rais Bush kuondoka madarakani.

Kama ilivyokuwa ikitarajiwa, hotuba yake imetilia mkazo juu ya vita dhidi ya ugaidi na silaha za kinyuklia na hapa rais Bush amezitetea seza zake dhidi ya ugaidi:

´´Kutenda sheria dhidi ya ugaidi sio kusababisha ugaidi. Ndio njia bora ya kuwalinda raia wetu. Hakuna sababu yoyote inayoweza kupelekea mauaji ya watu wasiokuwa na hatia yoyote. Hakuna nafasi ya ugaidi katika dunia ya leo´´.


Hasa juu ya suala la kinyuklia na lawama dhidi ya Iran na Korea ya kaskazini kwamba nchi hizo zimekaidi wito wa jumuiya ya kimataifa ya kusimamisha mipango yao ya kutengeneza silaha za kinyuklia, bila shaka rais Bush atakanushwa na rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad itakapofika zamu yake ya kukihotubia kikao hicho cha Umoja wa mataifa. Kwa muda wote Iran iliutetea mpango wake wa kinyuklia kwamba ni kwa ajili ya matumizi yake ya kijamii.


Rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy ambae ndie pia mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Ulaya, naye anatarajiwa kutoa hotuba yake. Kikao hicho cha mwaka cha Umoja wa mataifa mwaka huu kikiwa kimefanyika kukiwa na mzozo wa kifedha baada ya baadhi ya benki muhimu nchini Marekani kufilisika, tayari rais Nicolas Sarkozy ametoa wito viongozi wa benki na mashirika ya kifedha yaliyosababisha mgogoro wa kifedha wa sasa duniani wachukuliwe hatua kali.