1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Kikao cha Amerika Kusini na Asia Mashariki chataka kukamilishwa kwa Duru ya Doha.

Mawaziri wa mambo ya nje na wajumbe kutoka nchi 33 za Amerika ya Kusini na Asia ya Mashariki wametowa wito wa kukamilishwa kwa haraka mazungumzo ya Shirika la Biashara Duniani WTO ya Duru ya Doha kufuatia mkutano wao wa siku mbili uliofanyika katika mji mkuu wa Brazil Brasilia.

Waziri wa mambo ya nje wa Brazil Celso Amorium amesema taarifa ya mwisho ya Kikao hicho cha Ushirikiano wa Asia ya Mashariki na Amerika ya Kusini ambapo kwa ufupi hujulikana kama Fealac imesema licha ya tafauti ya maslahi yao ya biashara nchi hizo zimekuwa na dira ya aina moja ambayo inahitaji ufumbuzi wa haraka,wenye uwiano na wa mafanikio kwa mazungumzo ya Duru ya Doha.

Waziri wa mambo ya nje wa Japani Taro Aso hapo kabla alisema kikoa hicho kilikuwa kinaweza kutimiza dhima kubwa katika jukwaa la dunia.

Amesema kwa sababu Fealac ni kichocheo chenye nguvu kwa uchumi wa dunia ina majukumu mazito ya kushinikiza kwa nguvu mazungumzo ya Shirika la Biashara Duniani WTO kadhalika mageuzi ya Umoja wa Mataifa.

Washiriki wengi wa kikao hicho kama vile Brazil, China Indonesia au Argentina pia ni wanachama wa kundi la Mataifa 20 ya nchi zinazoendelea duniani ambazo zinapinga vikali ruzuku za kilimo zinazotolewa barani Ulaya na Marekani ambazo wanaziona kuwa sio haki.

Waziri wa mambo ya nje wa Ufilipino Alberto Romule ameliambia shirika la habari la AFP kwamba wanaamini Shirika la Biashara Duniani WTO ni muhimu lakini pia mashaka ya nchi zinazoendelea yanapaswa kushughulikiwa.

Mazungumzo ya shirika la biashara la biashara duniani yanayojulikana kama Duru ya Doha yenye lengo la kuondowa vikwazo vya biashara duniani yamekwama kwa miaka sita baada ya kuzinduliwa katika mji wa Qatar hapo mwaka 2001.

Mazungumzo hayo ya Duru ya Maendeleo ya Doha ya kuregeza masharti ya biashara yanakusudia kimsingi kupunguza ruzuku na ushuru wa kuingiza bidhaa ili kuzisaidia nchi zinazoendelea kunufaika na fursa ya biashara ya dunia inayotanuka.

Lakini nchi wanachama wa WTO zimeshindwa kuondokana na kikwazo juu ya kiwango cha punguzo hilo katika bidhaa za kilimo, viwandani na utowaji wa huduma kutokana na kuhitilafiana sana.

Nchi zinazoendelea zimekuwa zikishutumu nchi tajiri zikiongozwa na Marekani hususan kwa kulinda sekta yake ya kilimo.

Mkutano huu wa tatu wa Fealac ambao awali ulizinduliwa Chile hapo mwaka 2001 umemamilizika hapo Alhamisi kwa mazungumzo yasio rasmi yaliolenga kishindo cha hivi karibuni cha mikopo duniani na kuyumba kwa masoko ya dunia.

Waziri wa mambo ya nje wa Korea Kusini amekaririwa akisema kwamba tatizo hilo kwa kiasi fulani hivi sasa limedhibitiwa lakini bado halikumalizika na kwa hiyo ameyataka mataifa hayo yawe macho.

Kikao hicho pia kimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika biashara kati ya pande hizo mbili ambayo imefikia kwenye takriban dola trilioni moja hapo mwaka 2005.

Taarifa yao ya mwisho pia imegusia wasi wasi juu ya kuongezeka kwa pengo kati ya matajiri na maskini kadhalika kuongezeka kwa ujoto duniani.

Nchi wanachama wa Ushirikiano wa Amerika Kusini na Asia Mashariki kwa upande wa Asia ni Australia, Brunei,Cambodia China,Indonesia, Japani,Korea,Laos,Malaysia,Myanmar,New Zealand,Ufilipino Singapore,Thailand na Vietnam.

Kwa upande wa Amerika Kusini kuna Argentina,Bolivia,Brazil Colombia,Costa Rica,Cuba,Chile,Equador,El Salvador,Mexico Panama,Paraguay,Peru,Uruguay na Venezuela.

Mkutano wao ujao utafanyika baada ya kipindi cha miaka mitatu mjini Tokyo Japani.

 • Tarehe 24.08.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHjb
 • Tarehe 24.08.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHjb