1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiir aunga mkono kujitenga kwa Sudan Kusini.

2 Novemba 2009

Chama kinachotawala nchini Sudan- Sudanese National Congress kimesema kimesikitishwa na matamshi ya kiongozi wa Kusini mwa Sudan, kutaka eneo hilo lijitenge pale Sudan Kusini itakapoanda kura ya maoni mwaka wa 2011.

https://p.dw.com/p/KLVT
Kiongozi wa Kusini mwa Sudan Salvar Kiir, azungumza na Rais wa Sudan Omar el-Bashir.Picha: picture-alliance/dpa/dpaweb

Matamshi ya Salvar Kiir ya kutaka kusini mwa Sudan iwe taifa huru yanakuja wakati Wasudan kwa jumla wameanza kujiandikisha kupiga kura katika uchaguzi wa kwanza, kufanyika nchini humo katika muda wa miaka 20 ambao unazishirikisha pande zote mbili- kusini na kaskazini.

Kiongozi wa eneo la kusini mwa Sudan Salvar Kiir ambaye pia ni makamu wa pili wa rais nchini Sudan alikuwa anahudhuria misa ya Jumapili huko Juba, alipotoa matamshi ambayo sasa yamezua utata nchini Sudan.

Politik Sudan Konflikte Teilabkommen für Friedensvertrag in Sudan unterzeichnet
General Mohammed Hassan El-Farrow (L) wa Sudan ashikana mkono na Kamanda wa SPLM Taban Deng, baada ya kutiwa makubaliano ya amani.Picha: dpa

Salvar Kiir aliwaambia wananchi wa kusini mwa Sudan kwamba iwapo watapiga kura ya ndio kuunga mkono kuendelea kuwa chini ya Sudan katika kura ya maoni iliyopangwa kufanyika mwaka 2011,huko Sudan Kusini, basi hatma yao ni kwamba watasalia kutothaminiwa- na kwamba daima raia wa Kusini mwa Sudan watakuma nyuma ya wenzao wa Kaskazini.

Hii ndio mara ya kwanza Salvar Kiir ametamka wazi, msimamo wake wa kutaka eneo la kusini kujitenga na kuwa taifa huru kutoka serikali ya Khartoum ambaye yeye ni moja wa viongozi, kutokana na kwamba anashikilia wadhifa wa makamu wa rais wa pili.

Kama ilivyotarajiwa, matamshi ya Kiir hayakupokelewa vyema na serikali ya Omar El-Bashir. Chama tawala nchini Sudan Sudanese National Congress kilijibu matamshi ya Kiir kikisema wamesikitishwa na msimamo wa kiongozi huyo, na kwamba matamshi ya kujitenga kwa kusini mwa Sudan yanakiuka yale makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwaka 2005.

Eneo la Kusini mwa Sudan na Waislamu wa Kaskazini walipigana katika vita vya miongo miwili, hadi walipotia saini makubaliano ya amani miaka minne iliyopita, yaliyosababisha kugawana madaraka. Mojawapo ya masharti ya makubaliano hayo ilikuwa kufanyika kwa uchaguzi mwaka ujao na kura ya maoni mwaka 2011 kuhusiana na uhuru wa kusini mwa Sudan.

UN Sudan Präsident Omar el Bashir
Rais wa Sudan Omar el-Bashir.Picha: AP

Chama kinachoongozwa na Salvar Kiir, Peoples Liberation Movement wamesusia vikao vya bunge, kuishinikiza serikali kuwasilisha miswada kadhaa muhimu bungeni ikiwemo mswada wa kufanyia mageuzi idara muhimu ya upelelezi ambacho ni chombo muhimu katika uchaguzi wa mwakani.

Maafisa kutoka Kaskazini na Kusini wameshakubaliana kuhusu mbinu zitakazotumiwa kuanda kura hiyo ya maoni, lakini maafisa wa kusini mwa Sudan wanaishtumu Khartoum wakidai inawapa silaha wapiganaji huko kusini ili kulitia katika mvutanano na mgogoro eneo hilo kabla ya kufanyika kwa kura hiyo ya maoni.

Mzozo huu mpya nchini Sudan unafanyika wakati wasudan wameanza kujiandikisha kushiriki katika uchaguzi mkuu wa kwanza, utakaofanyika nchini humo katika muda wa miaka 20.

Katika uchaguzi huo utakaofanyika katika miezi sita ijaayo, raia nchini Sudan watamchagua rais na wawakilishi wao bungeni. Baada ya miaka 20 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, uchaguzi wa Aprili mwakani utakuwa zoezi la kwanza raia wa nchi hiyo watashiriki kwa mara ya kwanza.

Mwandishi: Munira Muhammad/DPAE

Mhariri: Abdul-Rahman