1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kifo cha Osama kimeibua hisia mbalimbali duniani kote

Admin.WagnerD2 Mei 2011

Kifo cha kiongozi wa wa Al-Qaeda Osama bin Laden kimeendelea kuibua hisia mbalimbali kote ulimwenguni. Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amesema kuuwawa kwa kiongozi huyo ni ushindi kwa wapenda amani.

https://p.dw.com/p/117lm
Osama bin Laden enzi za uhai wakePicha: AP

Katika taarifa yake ya pongezi kwa Rais Barack Obama Bibi Merkel amesema jeshi la Marekani limefanikisha ushindi mkubwa dhidi ya mtandoa wa kigaidi wa Al-Qaeda huku akihimiza kuendelea kuwa makini zaidi na matukio ya kigaidi.

Belgien EU Gipfel Angela Merkel in Brüssel
Kansela Angela Merkel wa UjerumaniPicha: dapd

Bibi Merkel alisema"Nimefurahi kusikia kwamba bin Laden ameuwawa, naamini ni jambo ambalo si Marekani tu, bali hata hapa Ujerumani limepokelewa vyema kwamba kiongozi wa mtandao wa kimataifa wa ugaidi, ambao umepoteza maisha ya watu wengi hawezi kuwa tena kitisho."

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle katika taarifa yake aliyoiita kifo cha "mmoja kati ya magaidi sugu duniani" amesema ni habari njema kwa wapenda amani na uhuru wa fikra.

Uingereza na Ufaransa nazo zimesema kifo cha Osama bin Laden hakiwezi kuondoa kitisho cha ugaidi na kuzitaka nchi za magharibi kuwa makini zaidi kukabiliana na mashambulizi ya kulipiza kisasi hasa katika kipindi hiki cha kushangilia kuuwawa kwake.

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa amesema kifo hicho ni mapinduzi makubwa katika vita dhidi ya ugaidi huku waziri mkuu wa Uingereza, David Cameron akisema nchi hiyo itaimarisha ulinzi katika wiki kadhaa kuanzia sasa.

Jeshi la Marekani, limemuuwa bin Laden katika operesheni iliyofanyika usiku wa kuamkia leo na kukamilisha msako mkali wa mtuhumiwa huyo aliyepanga mashambulizi ya Septemba 11 mwaka 2001.

Saudi Arabia imesema ina matumaini kwamba hatua hiyo itaongeza jitihada katika vita vya kupambana na ugaidi.

Taarifa iliyotolewa na Shirika la Habari la Saudi Arabia, inaeleza kuwa watu wa nchi hiyo walikuwa walengwa, ikitolea mfano wa tawi la al- Qaeda ambalo lilikuwa na makazi yake nchini humo.

Osama alivuliwa uraia wa Saudi Arabia baada ya kukosoa familia ya kifalme kutegemea vikosi vya Marekani baada ya Iraq kuivamia nchi jirani ya Kuwait.

Nayo Serikali ya Iran imesema kifo cha Osama kimeondoa sababu ya Marekani na washirika wake kupeleka majeshi katika nchi za mashariki ya kati kwa madai ya kukabiliana na ugaidi.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ramin Mehmanparast amesema Iran ilishiriki katika hatua za mwanzo za kumsaka Osama Bin Laden baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001 lakini ilijiondoa mapema baadaye kwa kusema operesheni hiyo inazuia kufikiwa suluhu yoyote kwa njia ya mazungumzo.

Hata hvyo kumekuwepo wanaolaani kuuwawa kwa Osama, kama kundi la Hamas la Ukanda wa Gaza, huku wanamgambo wa kundi la Taliban wakiapa kulipiza kisasi kuanzia kwa serikali ya Pakistan na baadaye Marekani.

Mwandishi: Sudi Mnette /RTR/AFP

Mhariri: Josephat Charo