1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KHARTOUM:Kiongozi wa kundi la JEM atishia kugomea mkutano wa Libya

7 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7Hv

Kiongozi muhimu wa kundi la waasi wa Darfur la Haki na usawa JEM ametishia kuugomea mkutano wa amani uliopangwa kufanyika nchini Libya baadae mwezi huu.

Khalil Ibrahim amesema katika mahojiano na kituo kimoja cha redio kwamba hatahudhuria mkutano huo ikiwa zaidi ya makundi mawili ya waasi wapinzani wake yataalikwa. Kiongozi huyo wa waasi aidha amesema kamati ya usuluhisi ya Umoja wa mataifa na Umoja wa Afrika inajivuta na imeandaliwa vibaya kwa mazungumzo hayo ya tarehe 27.Mazungumzo ya mwanzo yaligubikwa na migawanyiko ya waasi.Kundi moja tu kati ya makundi matatu ya waasi yaliyoshiriki lilitia saini makubaliano ya mwaka 2006 ambayo hayajatekelezwa.Tangu wakati huo waasi wamegawika katika makundi zaidi ya darzeni yanayopingana.

Wakati huohuo Mjumbe wa Marekani nchini Sudan ameelezea wasiwasi wake juu ya makubaliano ya amani ya miaka miwili yaliyomalizza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan.Andrew Natsios amesema hali ni tete kati ya serikali ya kaskazini na kusini mwa Sudan.Ameongeza kusema kuna umuhimu wa suala hilo kushughulikiwa kabla mambo hayajaharibika zaidi.