1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KHARTOUM : Sudan kutokabidhi raia wake kushtakiwa nje

4 Machi 2007
https://p.dw.com/p/CCMg

Rais Omar Hassan al Bashir hapo jana amesisitiza kwamba Sudan haitomkabidhi raia yoyote yule wa Sudan kwa ajili ya kushtakiwa nje ya nchi na mahkama za kimataifa kama vile Mahkama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC ambayo wiki hii imewashutumu Wasudan wawili kwa unyama uliotendeka Dafur.

Rais Bashir amekaririwa na shirika la habari la serikali SUNA akisema kwamba vyombo vya sheria vya Sudan ni vya uadilifu na vina sifa zinazostahiki kumshtaki Msudani yoyote yule ambaye ametenda uhalifu dhidi ya ubinaadamu.Amesema serikali haitomkabidhi raia wake kwa ajili ya kushtakiwa nje ya nchi.

Sudan inakibiliwa na shinikizo zito juu ya suala la Dafur baada ya Mahkama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC mjini The Hague Uholanzi wiki hii kumshutumu waziri mmoja mdogo na mwanajeshi wa vikosi vya ulinzi nchini Sudan kwa kuhusika na uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu kwa ukatili uliofanyika katika jimbo la Dafur.