1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Khamenei: Iran kuiunga mkono Syria hadi mwisho

5 Septemba 2013

Kiongozi mkuu wa kidini wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, amesema Marekani inayatumia mashambulizi ya kemikali nchini Syria kama kisingizio cha kuivamia nchi hiyo inayokabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

https://p.dw.com/p/19ch4
Kiongozi wa kidini Iran, Ayatollah Ali Khamenei
Kiongozi wa kidini Iran, Ayatollah Ali KhameneiPicha: picture-alliance/dpa

Aidha, ameionya Marekani kutokana na hasara itakazopata iwapo itafanya uvamizi wowote ule. Ama kwa upande mwingine, Umoja wa Ulaya umelipinga suala la kuivamia Syria kijeshi.

Akizungumza kwenye mkutano wa baraza la wataalamu, Khamenei amesema kuwa Marekani inajifanya kujiingiza katika mzozo wa Syria kwa kuzingatia zaidi suala la hali ya kibinaadamu na kwamba mashambulizi ya kutumika kwa silaha za kemikali, ni kama kisingizio kwao na kwamba nchi hiyo itajiingiza katika hasara kubwa iwapo itaivamia Syria kijeshi.

Iran kuendelea kumuunga mkono Rais Assad

Matamshi ya Khamenei yanaonyesha dalili za kutoacha kumuunga mkono mshirika wake wa karibu, Rais Bashar al-Assad, ambaye anashutumiwa na mataifa ya Magharibi kwa kutumia gesi ya sumu katika mashambulizi ya Agosti 21 mwaka huu dhidi ya raia. Kwa mujibu wa maafisa wa Marekani, kiasi watu 1,400 waliuawa katika mashambulio hayo.

Rais wa Syria, Bashar al-Assad
Rais wa Syria, Bashar al-AssadPicha: Reuters

Jana Jumatano (04.09.2013), mkuu wa kundi la Quds lenye mafungamano na Iran, Qassem Soleimani, aliliambia baraza la watalamu kwamba Iran itaiunga mkono Syria hadi mwisho.

Ama kwa upande mwingine, Urusi imeionya Marekani kwamba mashambulizi yoyote ya kijeshi dhidi ya Syria bila ya idhini ya Umoja wa Mataifa, yanaweza kuwa na madhara makubwa kama kombora litaangukia kwenye kiwanda kidogo cha madini ya uranium kilichoko karibu na Damascus.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi, imelitaka shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia masuala ya nyuklia, kutathmini haraka hatari itakayoweza kutokea, wakati Marekani inafikiria kuiadhibu serikali ya Syria kutokana na kuituhumu kutumia gesi yenye sumu.

Umoja wa Ulaya waizungumzia Syria

Wakati huo huo, Rais wa Umoja wa Ulaya Herman Van Rompuy na Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya, Jose Manuel Barroso, wamezungumza suala la kuivamia Syria kijeshi, huku wakiipinga hatua hiyo.

Viongozi wa EU, Herman Van Rompuy na Jose Manuel Barroso
Viongozi wa EU, Herman Van Rompuy na Jose Manuel BarrosoPicha: picture-alliance/dpa

Akizungumza leo na waandishi wa habari kabla ya kuanza kwa mkutano wa viongozi wa kundi la nchi zinazoongoza kiuchumi duniani-G20 unaofanyika mjini St. Petersburg, Van Rompuy amesema kuwa wanaheshimu wito wa Syria kuvamiwa kijeshi, lakini wanahitaji kuusogeza mbele mchakato wa Umoja wa Mataifa.

Kwa upande wake Barroso amesema jumuiya ya kimataifa haiwezi kukaa kimya baada ya kutokea kwa mashambulizi hayo ya Agosti 21 ambapo silaha za kemikali zinadaiwa kutumika na kutoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuitangaza mapema iwezekanavyo ripoti ya awali ya wakaguzi wa umoja huo.

Katika hatua nyingine kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Francis, amemuandikia Rais wa Urusi, Vladmir Putin barua, akitoa wito kwa viongozi katika mkutano huo kutafuta njia ya kuepusha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Syria, ambayo amesema hayana faida yoyote.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,DPAE,AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef