1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi ya Mubarak kusikilizwa upya Misri

Josephat Nyiro Charo13 Januari 2015

Mahakama ya rufaa ya Misri leo (13.01.2015) imebatilisha hukumu ya miaka 3 jela dhidi ya rais wa zamani, Hosni Mubarak, kwa mashitaka ya rushwa na kuamuru kesi pekee iliyobaki dhidi yake isikilizwe tena.

https://p.dw.com/p/1EJYw
ARCHIVBILD Hosni Mubarak
Rais wa zamani wa Misri, Hosni MubarakPicha: picture-alliance/AP Photo

Rais wa zamani wa Misri Hosni Mubarak ataendelea kubakia jela kwa wakati huu licha ya uamuzi wa mahakama kuu kubatilisha hukumu dhidi ya kiongozi huyo. Shirika la habari la Misri, MENA, limekinukuu chanzo cha habari katika wizara ya mambo ya ndani kikisema ingawa mahakama kuu imeamuru kesi ya ubadhirifu wa fedha dhidi ya Mubarak isikilizwe upya, haikuamuru aachiwe huru wala wanawe wawili wa kiume, wanaokabiliwa na mashitaka kama hayo.

Lakini duru za mahakama zinasema huenda Mubarak akawa huru hivi karibuni kwa kuwa hakuna mashtaka yaliyobaki dhidi yake kufuatia uamuzi wa mahakama. Hatua ya mahakama inafungua uwezekano wa Mubarak kuachiwa miaka minne tangu mapinduzi yaliyomuondoa madarakani.

Uamuzi wa kumuachia huru Mubarak sasa uko mikononi mwa ofisi ya muendesha mashtaka wa serikali au mahakama itakayoisikiliza upya kesi yake. Wafuasi wa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 86 walishangilia na kupiga kelele wakisema "Maisha marefu kwa haki" wakati mahakama ilipotangaza uamuzi wake.

Ni kinyume na sheria kuendelea kumzuia Mubarak

Wakili anayemtetea Mubarak, Farid al Deeb, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba mteja wake anatakiwa kuachiwa huru kwa kuwa tayari ametumikia miaka mitatu jela, pamoja na muda aliotumia akiwa kizuizini akisubiri kesi yake kusikilizwa. Deeb amesema Mubarak ataendelea kubakia hospitalini kwa kuwa ni mgonjwa.

Ägypten Mubarak Anklage fallengelassen jubelnde Anhänger
Wafuasi wa Mubarak wakishangilia CairoPicha: AFP/Getty Images/M. El Shahed

Mtaalamu wa sheria wa Mtandao wa kiarabu unaopigania haki ya kupata habari, Gamal Eid, amesema hakuna sababu yoyote kwa nini Mubarak aendelee kubakia kizuizini kwa kuwa tayari ameshatumikia muda wake au anakaribia kuumaliza na kwa mujibu wa sheria anaweza kuachiwa baada ya kutumikia theluthi mbili ya muda wake. Mtaalamu huyo aidha amesema, "Kuendelea kumzuia Mubarak ni kinyume na sheria. Wanaweza kumuachia bila kutangaza, lakini akibaki gerezani pengine itakuwa ni kwa sababu ya shinikizo la kisiasa."

Mwezi Novemba mwaka jana mahakama nyengine iliyafutilia mbali mashtaka dhidi ya Mubarak kuhusiana na vifo vya waandamanaji wakati wa maandamano ya msimu wa machipuko ya mwaka 2011 yaliyoufikisha kikomo utawala wake wa kiimla wa miongo mitatu. Makama ya chini ilikuwa imepitisha hukumu ya kifungo gerezani dhidi ya Mubarak mwezi Mei mwaka jana baada ya kumtia hatiani kwa ubadhirifu wa fedha zilizotengwa kwa ajili ya kuzifanyia matengenezo ikulu za rais.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/REUTERES

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman