1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kesi dhidi ya watuhumiwa wa uhalifu wa kivita nchini Kongo yaanza leo Stuttgart

4 Mei 2011

Kesi ya viongozi waasi wa Rwanda waliokamatwa nchini Ujerumani kwa madai ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imefanya dunia kuwa sehemu ndogo kwa washukiwa wa uhalifu.

https://p.dw.com/p/118cm
Ignace MurwanashyakaPicha: picture-alliance/ dpa

Siku ya Mei 4 majaji katika mji wa Stuttgart hapa Ujerumani wataanza kusikiliza ushahidi dhidi ya Ignace Murwanashyaka pamoja na Straton Musoni, Rais na makamu wa rais wa kundi la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda -FDLR.

Kundi hilo la FDLR limetawaliwa na kundi la wapiganaji wa Rwanda wenye asili ya Kuhutu ambao wamekuwa wakiendesha shughuli zao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, tangu mwaka 1994 na kwa kutumia majina mbalimbali.

Watuhumiwa hao walikamatwa Novemba 17, mwaka 2009 nchini Ujerumani ambako walikuwa wakiishi kwa miaka kadhaa na kwamba wanashtakiwa kwa makosa 26 ya uhalifu dhidi ya ubinadamu na makosa 39 ya uhalifu wa kivita ambayo yanadaiwa kufanywa na jeshi la FDLR katika ardhi ya Wacongo kati ya Januari mwaka 2008 na Novemba mwaka 2009. Wanadaiwa pia kujihusisha na kundi la ugaidi.

Kwa miaka kadhaa, kundi la wapiganaji la FDLR, limefanya mashambulio ya kikatili dhidi ya raia katika maeneo mengi ya mashariki mwa Congo, miongoni mwa waathirika walikuwa ni wanawake, watoto na wazee, na wengi kati ya hao walishambuliwa mpaka kufa kwa mapanga na majembe, huku wapiganaji hao waasi wakipora fedha na kuchoma nyumba, wakati mwingine wahanga hao wakiwa ndani wamefungiwa.

Marie ni mmoja ya wanawake waliokumbwa na masahibu hayo anasema waasi huwa wanakuja jioni katika makaazi yao, wakiwa makundi na kuingia nyumba hadi nyumba na hivyo inakuwa ngumu kwao kukimbia na kujiokoa kwa vile waasi wanakuwa pia wametapakaa maporini.

Shirika la haki za Binadamu la Human Right Watch linasema kuwa mashambuklio ya wapiganaji hao waasi mara nyingi yaliambatana na vitendo vya ubakaji.

Hata hivyo washtakiwa hao wawili hawakuwepo Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo wakati vitendo hivyo vya uhalifu vikifanyika, lakini wanajulikana kuwa walikuwa wakiwasiliana na kuagiza operesheni mbalimbali zilizokuwa zikifanywa na wapiganaji hao wa FDLR, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Kama viongozi waandamizi wa kundi hilo, wote wanabeba lawama za kuwajibika kwa uhalifu uliofanywa na wapiganaji hao, iwapo itaonekana kuwa waliagiza kufanyika kwa uhalifu huo au walijua juu ya uhalifu huo kufanyika na kwamba hawakufanya jitihada zozote kuzuia.

Imeelezwa kwamba wapiganaji hao wa FDLR walikuwa wakipata msaada kutoka nje, Ulaya, America kaskazini, na nchi za Afrika kwa kuwezeshwa kupata silaha, wapiganaji na fedha.

Mpaka sasa ghasia badio zinaendelea katika majimbo ya Kivu ya kusini na kaskazini mashariki ya Congo na kwamba kundi hilo la FDLR pamoja na makundi mengine ya wapiganaji yanaendeleza vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu dhidi ya raia, ambapo kwa mujibu wa duru za umoja wa mataifa na mashirika mengine ya kiutu, katika tukio la hivi karibuni wanawake 53 pamoja na wasichana walibakwa na wapiganaji hao wa FDLR kusini mwa Fizi, katika jimbo la Kivu ya kusini kati ya Januari 19 na 21.

Kesi hii ni ya kwanza kusikilizwa chini ya sheria ya ujerumani ya uhalifu iliyopitishwa Juni mwaka 2002, ambayo imeingiza uhalifu chini ya sheria ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu- ICC.

Mkurugenzi anayeshughulika na masuala ya sheria za utetezi kimataifa wa Shirika la Human Rights Watch Mattioli-Zeltner amesema kesi ya watuhumiwa hao Murwanashyaka na Musoni inatoa fursa kwa waathirika wa vitendo vya uhalifu vilivyofanywa na wapiganaji wa FDLR hatimae kuona haki ikitendeka baada ya miaka kadhaa ya mateso.

Mwandishi: Halima Nyanza (HRW press)

Mhariri:Abdul-Rahman