1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yaweka sheria kali dhidi ya dawa za kuongeza nguvu

12 Januari 2015

Wakuu wa riadha nchini Kenya wametangaza sheria kali za kukabiliana na visa vya matumizi ya dawa za kuongeza nguvu mwilini, ikiwa ni pamoja na kuwafanyia vipimo vya ghafla wanariadha maahiri

https://p.dw.com/p/1EIwp
Symbolbild Doping
Picha: Fotolia/gebai

Shirikisho la riadha la Kenya AK limesema hatua hiyo inaenda sambamba na sheria za Shirikisho la Riadha Ulimwenguni – IAAF na Shirika la Ulimwengu la Kupambana na Matumizi ya Dawa za kuongeza nguvu mwilini – WADA.

Mwenyekiti wa AK Isaiah Kipgalat amesema makocha wote na mawakala lazima wasajiliwe na shirikisho hilo. Kiplagat amesema shirikisho hilo litaanzisha warsha za mafunzo kote nchini ili kuwaelimisha wanariadha kuhusu athari za matumizi ya dawa hizo. Wanariadha wote mashuhuri watahitajika kusajiliwa na kupewa namabri ya leseni ifikapo mwezi Machi mwaka huu.

Rais wa Kamati ya Kenya ya Olimoiki Kipchoge Keino atakutana na Waziri wa Michezo Hassan Wario ili kuijadili sheria mpya ambayo huenda ikajumuisha vifungo vya jela kwa makocha au mawakala wanaohimiza matumizi ya dawa hizo.

Rita Jeptoo, mshindi mara tatu wa Boston Marathon na bingwa mara mbili wa Chicago Marathon, aligundulika kutumia dawa za kuongeza nguvu mwilini nchini Kenya mwezi Septemba. Na sasa ametakiwa pamoja na makocha na wakala wake kufika Alhamisi wiki hii mbele ya tume ya AK ya matibabu na kupambana na dawa za kuongeza nguvu ambayo itaisikiliza kesi hiyo

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/reuters
Mhariri: Josephat Charo