1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya yajiandaa kwa ziara ya Obama

Caro Robi20 Julai 2015

Maafisa nchini Kenya wako katika pilika pilika za kuunadhifisha mji mkuu wa nchi hiyo, Nairobi, kujitayarisha kwa ziara ya Rais wa Marekani Barack Obama. Kiasi kikubwa cha fedha kimetumika kwa ukarabati.

https://p.dw.com/p/1G1Vh
Mji mkuu wa Kenya, Nairobi
Picha: Fotolia/Natalia Pushchina

Kwa kipindi cha mwezi mmoja sasa, mamia ya wafanyakazi wa kaunti ya Nairobi wameajiriwa kuurembesha mji wa Nairobi kutokea uwanja mkuu wa ndege wa Jomo Kenyatta hadi katikati ya mji mkuu.

Wafanyakazi hao wanazifanyia ukarabati barabara za mji huo kupanda nyasi na maua kando mwa barabara, kufagia na kupaka rangi, yote hayo yakiwa ni sehemu ya maandalizi kabambe ya ziara rasmi ya Rais wa Marekani Barack Obama anayefanya ziara hiyo ya kwanza rasmi tangu kuwa rais wa Marekani mwaka 2009.

Shughuli hizo za kuukarabati na kuunadhifisha mji wa Nairobi zimesababisha msongamano hata zaidi wa magari katika barabara kuu za mji huo na kuwa kero kwa baadhi ya wakaazi wa mji huo. Wengi wa wakaazi hao wameghadhabishwa na uongozi wa kaunti ya Nairobi chini ya usimamizi wa gavana wa jimbo hilo Evans Kidero kuwa wanasubiri hadi Obama kuja Kenya ndipo waufanyie ukarabati mji huo. Hata hivyo wengi wao wamefurahishwa na ujio huo wa Obama ambaye baba yake ni Mkenya.

Wajasiriamali wakutana Nairobi

Serikali ya mitaa ya Nairobi imesema inatumia kiasi cha euro 400,000 kuufanyia ukarabati mji huo. Wakosoaji wanasema ukarabati huo unafanywa kwa majengo machache tu na njia atakayotumia kiongozi huyo wa Marekani.

Msongamano wa magari umeongezeka Nairobi wakati wa maandalizi
Msongamano wa magari umeongezeka Nairobi wakati wa maandaliziPicha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Siku ya Alhamisi, Rais Obama anatarajiwa kutua nchini Kenya kuhudhuria mkutano wa kilele wa kimataifa wa wajasiriamali unaofanyika mjini Nairobi.

Mkutano huo ujulikanao kwa kifupi GES unalenga kuimarisha biashara ambazo zinatoa matumaini za kuwasaidia waafrika kuondokana na umasikini na kusaidia katika kukabaliana na ongezeko la kuwepo itikadi kali miongoni mwa jamii kutokana na ukosefu wa ajira.

Obama kutembelea Ethiopia pia

Miongoni mwa mada zinazotarajiwa kupewa kipaumbele katika ziara hiyo ni masuala ya kibiashara na usalama. Kabla ya ziara hiyo, Obama amesema ziara yake nchini Kenya ina umuhimu mkubwa na atatoa ujumbe kuwa Marekani ni mshirika mkubwa sio tu kwa Kenya bali kwa kanda ya jangwa la sahara barani Afrika.

Rais Obama pia anatarajiwa kufanya ziara nchini Ethiopia akiwa Rais wa kwanza wa Marekani kuizuru Ethiopia, ambako atayazuru makao makuu ya Umoja wa Afrika yaliyoko mjini Addis Ababa na kufanya mazungumzo na viongozi wakuu wa umoja huo ambako masuala ya nafasi ya demokrasia barani Afrika yanatarajiwa kujadiliwa.

Zaidi ya makundi 50 ya Afrika na ya kimataifa ya kutetea haki za binaadamu yakiwemo ya Human Rights Watch na Freedom House yamemuandikia Obama yakimtaka kupeleka ujumbe wa kuwepo demokrasia barani Afrika.

Mwandishi:Caro Robi/afp

Mhariri:Josephat Charo