1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya: mbinyo wa kimataifa kubakia

18 Januari 2008

Kenya inashuhudia leo siku ya 3 ya maandamano ya upinzani wanaodai uchaguzi mpya.Vipi kumaliza balaa la Kenya ?

https://p.dw.com/p/CtUj
Rais Kibaki ***Picha: AP Photo

Licha ya mkomoto unaoendeshwa na polisi,upinzani nchini Kenya unaendelea tena hii leo na maandamano yake dhidi ya serikali ya kutatanisha ya rais Mwai Kibaki.Kwa muujibu wa taarifa tofauti ,kati ya watu 10 hadi 20 wameuwawa hadi sasa katika maandamano haya.

Wafuasi wa Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga wanaituhumu serikali kupitisha mizengwe katika uchaguzi.Dai lao la kuitishwa uchaguzi mpya linaungwamkono hata na Umoja wa Ulaya.

Jambo moja ni dhahiri kabisa: serikali ya kutatanisha ya kenya hadi sasa imeonesha haijali mbinyo wa kimataifa.Kwanza ilizima juhudi zote za upatanishi za Umoja wa Afrika (African Union) na zile za waziri mdogo wa mambo ya nje wa Marekani Jendayi Frazer na hivi punde imesema haijali hata vikwazo vya Umoja wa Ulaya.

Akijibu uamuzi wa Umoja wa Ulaya unaodai uchaguzi urudiwe na kuitishia kuzuwia msaada wowote kwa Kenya,msemaji wa serikali ya Kenya, Alfred Mutua alisema serikali ya Kenya haikubali kutishwa.Kenya haina haja ya upatanishi wa kimataifa.

Wakati Upinzani umepanga kuendelea hata leo ijumaa na maandamano kote nchini yaliochukua -kwa muujibu wa upinzani-maisha ya watu 20,mkomoto wa polisi umezidi kupambamoto wakitumia hewa ya kutoa machozi,virungu na hata risasi.

Yadhihirika, rais anaebishwa Mwai Kibaki anapitisha tu wakati akitumai mzozo huu utatoweka wenyewe.Kuzidi kupungua kwa wale wanaoshiriki maandamano kunamfanya aamini mkakati wake unafanya kazi. Hofu za mkomoto wa vikosi vya usalamana mvua kali zinazonyesha Kenya,yamkini yaweza kuwa pia sababu ya kutoshiriki kwa wingi kwa umma mkubwa kwenye maandamano.

Katika mashina ya Upinzani huko magharibi mwa nchi hii ya Afrika Mashariki,serikali hivi sasa inajaribu kuwatisha wafuasi wa Upinzani kwa msaada wa kurundika huko majeshi mengi.

Kuanzia wiki ijayo,Upinzani umepanga mkakati mpya: Umepanga kuanzisha migomo na kuyasusia makampuni yalio mali ya vigogo vinavyomzunguka rais Kibaki.

Swali linaloibuka:vipi Kibaki anapanga kuitawala Kenya ? muungano wake wa vyama PNU una viti 43 tu Bungeni wakati Upinzani ODM una jumla ya viti 99.

Wakati wa uchaguzi wa spika wiki hii,ambae kwa muujibu wa katiba ya Kenya- baada ya rais na makamo-rais ni mtu 3 mwenye madaraka makuu-ushindi ulikwenda kwa chama cha ODM.Kilinyakua pia wadhifa wa makamo-spika.Na hii yadhihirisha dhahiri-shahiri,Upinzani una uiwezo wa kutia munda mpango wowote ule wa serikali.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga kama hapo mwanzo angali anapendelea upatanishi wa kimataifa juu ya mzozo huu na ikibidi, kuwekewa Kenya hata vikwazo zaidi.

Anamnyoshea mkono rais Kibaki waunde serikali ya muungano ambayo iandae mnamo muda ama wa miezi 3 au 6 uchaguzi mpya.

Swali hapa ni iwapo , kule kupatanisha kulikoahirishwa kwa Katibu Mkuu wa zamani wa UM Kofi Annan kutaendelea au yeye ana nguvu zaidi za uptanishi kuliko wapatanishi waliomtangulia ?

Hasira na ghadhabu za wananchi juu ya hatima yao zinazidi....Imani ya wananchi kwa wanasiasa na kwa uchaguzi usio na mizengwe imetoweka.Ili kumaliza maafa ya wakenya kiasi cha 500.000-kwa muujibu wa taarifa za UM wanaohitaji msaada wa chakula,ni dharura kabisa kwa Jumuiya ya kimataifa tena kwa nguvu zake zote upiganie uchaguzi mpya na kurejesha suluhu nchini Kenya.

Wakati unapita na hata kwa jicho la kiuchumi.Kwani, michafuko hadi sasa imesababisha hasara ya kiasi cha dala bilioni 1 na kwa majirani wanaotegemea bidhaa zinazoagizwa kutoka nje,kila siku zaidi balaa hili linaendelea, ni msiba !