1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya kuwafukuza madaktari wanaogoma

Admin.WagnerD14 Desemba 2016

Wizara ya afya ya Kenya imewaonya madaktari wanaogoma kwa wiki ya pili sasa, kwamba wanaweza kufutwa kazi, na viongozi wa chama chao wakafunguliwa mashitaka. Madaktari wamesema hivyo ni vitisho.

https://p.dw.com/p/2UGL6
Kenia Ärzte Protest
Madaktari wanaogoma wakiandamana KenyaPicha: Reuters/T. Mukoya

Serikali ya Kenya imetishia kuwafukuza kazi madaktari wanaogoma ikiwa hawatarejea kazini, na maafisa wakuu wa chama chao kukamatwa na ku­­­shtakiwa kwa kukiuka agizo la mahakama. Madaktari na wauguzi wamekiuka agizo lililotolewa na mahakama siku ya jumatatu na kuapa kuendelea na mgomo huo.

Mnamo siku ya Jumapili chama cha wauguzi kilitia saini makubaliano ya kurejea saini kati yao na serikali, mkataba ambao baadaye katibu mkuu wa chama hicho aliukana na kusema mgomo wa wauguzi bado unaendelea.

Katibu Mkuu huyo Seth Panyako alisema, "Agizo hilo la mahakama lilitolewa bila kuzingatia uwakilishi na watu waliowasilisha kwa hivyo hakuna kanuni za kisheria na kwa hivyo hakuna agizo halali la mahakama kusimamisha mgomo wa wauguzi unaoendelea.''

Madaktari wapuuza kitisho

Madaktari wameapa kuendelea na mgomo wao na kusema hawatishiki kuachishwa kazi. "Ukiwadharau Madaktari ina maana kwamba huwahitaji kwa hivyo usituambie turudi kazini.” Amesema Katibu mkuu wa chama cha Madaktari Nchini Dr. Ouma Oluga.

Anschlag in Lamu (Kenia)
Wagonjwa ndio wanaopata taabu kubwa kutokana na mgomo huuPicha: Reuters

Serikali mjini Nairobi imetishia kuwakamata viongozi wa chama cha madaktari kwa kukiuka agizo la mahakama. "Tunahitaji kufahamu sheria inasema nini na tunahitaji kuheshimu sheria kwani hakuna yeyote aliye mkuu kushinda sheria,” ameonya Katibu katika Wizara ya Leba Phillis Kandie.

Wapiganapo ndovu, nyasi huumia

Mgomo huo umelemaza shughuli za huduma za afya huku madaktari wa hospitali za kibinafsi wakitishia kujiunga nao.

Katibu Mkuu wa chama cha Madaktari Dr. Oluga amesema Madaktari wanaongea sio kama madaktari bali kama wakenya, ''na kama wakenya sisi ndio tumeajiri serikali ni sharti itekeleze mkataba wa makubaliano na tulipwe marupurupu yetu”.

Kwa sasa wagonjwa katika hospitali  kuu za umma wanahudumiwa na madaktari kutoka idara ya jeshi.

Mgomo huo umeingia wiki ya pili sasa huku zaidi ya vifo vya wagonjwa 30 vikiripotiwa katika hospitali mbali mbali za umma kuhusiana na mgomo huo.

Alfred Kiti DW - Nairobi.

Mhariri: Grace Patricia Kabogo