1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya kufungiwa nje ya Michezo ya Olimpiki?

1 Aprili 2016

Kuna wasiwasi huenda Kenya ikakosa kutunga sheria ya kupambana na matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni, kabla ya kumalizika muda wa mwisho uliowekwa Shirika la Kimataifa la WADA, wa Aprili 5

https://p.dw.com/p/1IOE2
Olympia London 2012 3000 Meter Hindernis
Picha: Reuters

Kwa kushindwa kufanya hivyo, ina maana huenda Kenya ikafungiwa nje ya michezo ya Olimpiki ya Rio. Mswada unaolenga kufanya matumizi ya dawa za kuongeza nguvu za misuli kuwa kosa la jinai, ulijadiliwa kwa mara ya kwanza bungeni mwishoni mwa wiki hii, lakini kwa sasa bunge liko katika mapumziko kwa siku kumi zijazo, hadi baada ya muda wa mwisho wa Aprili 5. Mswada huo utapaswa kuwasilishwa tena katika vikao viwili, kujadiliwa na kamati bunge, na kuidhinishwa na rais kuwa sheria, mchakato ambao unaweza kuchukua miezi kadhaa.

Na hata wakati kukiwa na wingu la sintofahamu kuhusu nafasi ya Kenya kushiriki katika Olimpiki, wanariadha wakimbizi wenye ndoto ya kupata kibali cha kwenda Rio mwezi Agosti katika mashindano hayo wanaendelea kuyanoa makali katika Milima ya Ngong nchini Kenya.

Wanariadha hao walichaguliwa kutoka kambi tofauti za wkaimbizi Kenya – ikiwemo ya Daadab, kubwa kabisa duniani, na Kakuma – kujiunga katika kambi ya mazoezi nje kidogo ya mji mkuu Nairobi. Miongoni mwa wanatokea Congo, Somalia, na Sudan Kusini. Angelina Ndai ni mwanariadha mkimbizi kutoka Sudan Kusini "Kwangu mimi ntajivunia saan kuwa pale na kutambuliwa kuwa Msudan Kusini kwa sababu Wasudan Kusini wengi hawajawahi kuwa katika mashindano ya dunia lakini mwaka huu angalau mmoja ataweza kuwakilisha"

Wanamichezo na walimu wao wana matumaini ya kufanya vyema katika Olimpiki. Kocha wa zamani wa timu ya Kenya John Anzrah ndiye aliye na jukumu la kuwaandaa wanariadha wakimbizi. "Walikuja wakati hawana ujuzi wowote, lakini sasa tumewanoa makali, wanaweza kukimbia kama wanariadha wanaopata mafunzo. Tofauti pekee ni kuwa wengine ni maarufu na hawa wanafuata nyayo zao".

Mkuu wa kamati ya Olimpiki ya Kenya na mwanachama wa bodi ya Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki – IOC Kipchoge Keino, amesema wanariadha hao lazima waandikishe muda bora wa kufuzu ili wachaguliwe kwenye timu. "Nadhani ni muhimu kwa hao wakimbizi kushiriki nchi wanazotoka zitaona zina kipaji ambacho kimeanzishwa na zitahitaji kukaa kwenye meza na kuwarejesha nyumbani watu wao ili wawe sehemu ya nchi yao".

Watakochaguliwa wataingia uwanjani katika shereze ua ufunguzi wa Olimpiki wakiwa na bendera ya nembo ya Olimpiki, na kupigwa wimbo wa rasmi wa Olimpiki ili kuwatambulisha kuwa wanariadha na sio tu wakimbizi. Uamuzi wa mwisho utatolewa Juni. Timu ya wanariadha wakimbizi inatarajiwa kuwajumuisha wanariadha watano hadi kumi kutoka kote ulimwenguni, ikiwa ni sehemu ya ahadi ya IOC “kuwasaidia wanamichezo wenye uwezo na ambao wanaathiriwa na mgogoro wa wakimbizi kote duniani”.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Khelef