1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Katibu Mkuu Ban Ki-moon aendelea na ziara Sudan

4 Septemba 2007

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon anaendelea na ziara yake nchini Sudan ameenda kusini mwa nchi hiyo kwa lengo la kuunga mkono makubaliano ya kudumisha amani kati ya Sudan ya kusini na kaskazini.

https://p.dw.com/p/CH8X
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moonPicha: AP

Katibu Mkuu Ban Ki–moon anaenda kusini mwa Sudan kwa lengo la kuunga mkono makubaliano ya amani yaliyomaliza vita baina ya sehemu hiyo na kaskazini vilivyochukua muda wa miaka 21. Umoja wa Mataifa umeweka askari alfu 10 ili kulinda amani katika sehemu hiyo .

Katika tamko , katibu Mkuu Ban Ki-moon amesema ziara yake nchini Sudan ni ishara ya kusisitiza dhamira ya kuunga mkono makubaliano ya amani na kwamba katika muda wake wote kama katibu mkuu amekuwa anasuburi kwa hamu wasaa wa kukutana na viongozi wa Sudan na hasa rais Oumar Bashir ili kujadili njia za kutekeleza makubaliano ya kuleta amani na usalama.

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanaongozana na katibu mkuu pia wamesema kuwa bila ya amani ya kudumu baina ya Sudan za kaskazini na Kusini haitawezekena kutatua mgogoro wa jimbo la Darfur.

Katika ziara yake kwenye jimbo la kusini bwana Ban Ki-moon anatarajiwa kukutana na aliekuwa kiongozi wa waasi bwana Salva Kiir ambaye ni makamu wa kwanza wa rais wa jimbo la kusini.

Mkataba wa amani uliomaliza vita vya miaka 21 baina ya kusini na kaskazini ulitiwa saini na kiongozi wa waasi wa hapo awali hayati John Garang. Lakini hatahivyo hali ya kusini bado haijakuwa ya kutengemaa jambo linalomtia wasiwasi katibu mkuu Ban Ki-moon.

Wadadisi wanasema ziara ya katibu mkuu Ban Ki- moon inaashiria wasiwasi mkubwa uliopo juu ya Sudan kusambaratika na kurejea katika mgogoro mkubwa sana. Msemaji mmoja ambae hakutaka kutajwa ameeleza kuwa wasiwasi huo upo miongoni mwa viongozi wa serikali ya Sudan.

Wakati huo huo bwana Ban Ki- moon ametangaza fanikio lake la kwanza katika ziara yake nchini Sudan.Baada ya mazungumzo yake na rais Oumar Bashir, rais huyo ameahidi kuwa kiongozi wa waasi katika jimbo la Darfur Suleiman Jamous ataruhusiwa kuondoka nchini ili kupata matibabu nje.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa bwana Ban Ki -moon anatarajiwa kuwasili katika jimbo hilo la Darfur, magharibi mwa Sudan hapo kesho na amesisitiza ulazima wa kupelekwa haraka askari alfu 26 wa Umoja wa Mataifa watakaolinda amani katika sehemu hiyo.

AM