1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Katiba mpya yaungwa mkono Misri

17 Desemba 2012

Rais Mohamed Mursi aungwa mkono na Wamisri katika duru ya kwanza ya kura ya maoni juu ya katiba mpya ambayo anataraji itaitowa nchi hiyo kwenye mzozo wakati wapinzani wakiipinga kwa kukandamiza haki za jamii ya wachache.

https://p.dw.com/p/173iP
Kura Maoni Misri
Kura Maoni MisriPicha: AP

 Katika siku ya kwanza ya kura ya maoni juu ya rasimu ya sheria za msingi za nchi hiyo asilimia 56.5 ya kura zimeikubali kwa kura ya ndio. Duru ya pili ya kura hiyo ya maoni hapo Jumamosi ijayo yumkini ikapiga kura nyengine ya ndio kutokana na maeneo mengi yanayotarajiwa kupiga kura hiyo yana wafuasi wa itikadi kali za Kiislamu na hiyo ina maana kwamba katiba hiyo itapita.Lakini wakati kura ya hapana ikiwa ni asilimia 43 jambo ambalo linaloonyesha kukaribiana kwa matokeo hayo hakumpi faraja kubwa Mursi kutokana na mgawanyiko mkubwa katika nchi ambapo anahitaji kuwa na muafaka kwa ajili ya kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi.

Muungano wa Ukombozi wa Taifa umesema hautotambuwa matokeo yoyote yale yasiyo rasmi na utasubiri matokeo ya mwisho baada ya kura ya duru ya pili. Umetowa wito kwa wananchi wa Misri kuandamana barabarani hapo Jumanne kutetea uhuru wao, kuzuwiya hujuma na kuikataa rasimu hiyo ya katiba.Pia umesisitiza kwamba kura ya maoni ya hapo jana imegubikwa na ukiukaji wa taratibu za kupiga kura.

Kura zikihesabiwa baada ya kumalizika zoezi la kura ya maoni mjini Cairo.
Kura zikihesabiwa baada ya kumalizika zoezi la kura ya maoni mjini Cairo.Picha: Reuters

Taratibu za kupiga kura zakiukwa

Mkuu wa muungano huo Mohamed El Baradei ambaye ni mkuu wa zamani wa Shirika la Nishati ya Nuklea la Umoja wa Mataifa amesema kupitia mtandao wa twitter kuhusu duru hiyo ya kwanza ya kura ya maoni kwamba nchi imegawika,taratibu za kupiga kura zimekiukwa,watu wachache wamejitokeza kupiga kura,hali ya kukatishwa tamaa na Waislamu wa itikadi kali imekuwa ikizidi kuongezeka na hali ya kutojuwa kusoma na kuandika inaendelea kuwa kikwazo nchini humo.Makundi kadhaa ya kutetea haki za binaadamu na yale yalioangalia kura hiyo yamesema kulikuwa na ukiukaji wa taratibu na kutaka kura hiyo irudiwe.Yamesema waangalizi waliondolewa kutoka baadhi ya vituo vya kupigia kura, majaji hawakuwepo, mahala pengine walionekana majaji wa bandia na kuna matukio ambapo wanawake walizuiliwa kupiga kura.

Nchi inaweza kutumbukia kwenye udikteta

Wakati huo huo waziri wa masuala ya maendeleo wa Ujerumani Dirk Niebel ameelezea wasi wasi wake juu ya hali hiyo ya Misri. Amesema ana hofu kwamba nchi hiyo chini ya Rais Mursi na Chama cha Udugu wa Kiislamu inaweza kutumbukia kwenye udikteta. Ujerumani imepunguza mawasiliano na serikali hiyo ya Misri na ule mpango wa msamaha wa madeni wa euro milioni 240 kwa nchi hiyo umesitishwa kwa sasa. Lakini wakati Misri itakapokuwa na demokrasia na uhalali wa katiba Ujerumani itatowa msaada wake kwa juhudi hizo.

Iwapo mchakato huo wa katiba utapita uchaguzi wa taifa unaweza ukafanyika mapema mwakani jambo ambalo wengi wanatumai litaleta utulivu ambao umekosekana nchini Misri tokea kuanguka kwa Hosni Mubarak takriban miaka miwili iliopita.

Mwandishi:Mohamed Dahman/RTRE

Mhariri:Josephat Charo