1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela wa Ujerumani ziarani Marekani

26 Juni 2009

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel baadae leo Ijumaa atakutana na Rais wa Marekani Barack Obama katika Ikulu ya Marekani mjini Washington.

https://p.dw.com/p/Ibfb
Bundeskanzlerin Angela Merkel gibt am Montag (22.06.2009) in Potsdam nach ihrer Teilnahme an der Konferenz der CDU/CSU-Fraktionsvorsitzenden aus den Bundesländern ein Pressestatement. Die Fraktionsvorsitzenden berieten über Fragen der Finanz- und Wirtschaftspolitik und über die Entschädigung von SED-Opfern 20 Jahre nach dem Mauerfall. Foto: Bernd Settnik +++(c) dpa - Report+++
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel.Picha: AP

Mtikisiko wa uchumi duniani na mabadiliko ya hali ya hewa ni mada kuu zitakazojadiliwa na viongozi hao wakati wa mkutano wao wa saa tatu. Rais Barack Obama na Kansela Angela Merkel kwanza watakuwa na mazungumzo ya faragha katika ofisi ya Obama na baadae watakuwa na majadiliano pamoja na wajumbe mbali mbali kama ilivyo desturi ya rais huyo wa Marekani anapokutana na viongozi wa kigeni. Hatimae bama na Merkel pamoja watakutana na waandishi wa habari kwenye bustani ya Ikulu kabla ya kula chakula cha mchana pamoja.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Robert Gibbs amesema, mzozo wa kisiasa nchini Iran,mipango ya kuimarisha uchumi ulioporomoka, nishati na mabadiliko ya hali ya hewa ni baadhi ya masuala yatakayojadiliwa. Rais Obama na Kansela Merkel watajitahidi kuwa na msimamo mmoja kabla ya mkutano wa viongozi wa nchi nane tajiri zilizoendelea kiviwanda G-8 uliopangwa kufanywa mwezi ujao nchini Italia.

Kwenye mkutano huo, nchi tajiri za kundi la G-8 zinatazamiwa kutoa mapendekezo juu ya namna ya kuboresha shughuli za masoko ya fedha na kusaka juhudi za pamoja kupambana na ongezeko la joto duniani, kabla ya mkutano wa kimataifa kuhusiana na hali ya hewa utakaofanywa mjini Copenehagen mwisho wa mwaka huu. Merkel ataitumia ziara yake ya saa 25 mjini Washington kuupigia debe mkutano huo ili usimalizike bila ya mafanikio thabiti kupatikana. Kansela Merkel kabla ya kuanza ziara yake alipuuza tofauti za maoni zilizoripotiwa na vyomba vya habari na badala yake alisisitizia mkondo mpya wa mwenyeji wake katika takriban kila sekta. Akaongezea:

"Ujerumani inafurahia hali hii. Tumeshabainisha msimamo wetu nchini Afghanistan katika kile kinachojulikana kama mtandao wa hatua za usalama unaoungwa mkono hivi sasa na Marekani.Na tutaendelea kuunga kama tutakavyoweza ili kuhakikisha matokeo ya maana yanapatikana kufuatia mkondo huu mpya."


Hata hivyo,serikali ya Obama ingependa kuiona Ujerumani ikitoa mchango mkubwa zaidi katika jitahada mpya za Marekani kuwatimua wanamgambo wa mwisho wa Taliban na Al-Qaeda kutoka Afghanistan. Vita vya Afghanistan vinapingwa vikali nchini Ujerumani na Merkel akikabiliwa na uchaguzi mkuu baadae mwaka huu, hawezi kupuuza maoni ya umma.

Mwandishi: T.Nehls /P.Martin

Mhariri: J.Charo