1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel kuizuru Uturuki

1 Februari 2017

Ni ziara nyeti wakati Kansela Angela Merkel wa Ujerumani atakapoizuru Uturuki Alhamisi ikiwa ni ziara ya kwanzal tokea nchi hiyo ilipozima jaribio la mapinduzi.

https://p.dw.com/p/2WoMJ
Bildkombo Angela Merkel Recep Tayyip Erdogan
Picha: picture-alliance/dpa/Sagolj/Zivulovic/Kombo

Maelfu ya wanasiasa wa upinzani,waandishi wa habari, waendesha mashtaka na raia wa kawaida wametiwa mbaroni. Vyombo vya habari vyenye kuikosoa serikali vimefungwa na muungano wa upinzani wa Wakurdi umevunjwa.Daima tuhuma zinakuwa na zile zile: kwamba watu hao walikuwa wameshiriki katika jaribio hilo la mapinduzi lililoshindwa. Serikali ya Uturuki imekuwa ikiwaandama wafuasi wa vuguvugu la Gülen kwa kuwahusisha na jaribio hilo la mapinduzi. Shutuma za kimataifa zimerudi tena kama kawaida kuishutumu serikali ya wahafidhina wa Kiislamu ya chama cha ACP kwa ukandamizaji wake.Uturuki nayo imejibu shutuma hizo kwa kuituhumu Ujerumani kwa kushindwa kuonyesha mshikamano wake katika mapambano dhidi ya ugaidi.Halikadhalika Ujerumani inadaiwa kuwapatia eneo la kukimbilia na fedha wapiganaji wa  Chama cha Wakurdi kilichopigwa marufuku (KKP).

Hakuna ishara nzuri kwa ziara hiyo ya Merkel nchini Uturuki. Wanasiasa wengi wa upinzani nchini Ujerumani wanaiona ziara hiyo inatowa ishara mbaya kabisa.Kwa mwanasiasa wa sera za mrengo wa kushoto Sevim Dagdelen ziara hiyo ya Merkel imekuja wakati sio muafaka.

Kuwepo kwa Kansela Merkel nchini Uturuki ikiwa ni wiki chache kabla ya kufanyika kura ya maoni kuhusu mabadiliko ya katiba nchini humo kunachukuliwa na wapinzani kama ni kumuunga mkono Rais Tayyip Erdogan, ambaye chama kilianzisha mchakato huo unaonuwia kuiongezea madaraka zaidi ofisi ya rais.

Naye mwanasiasa wa chama cha watetezi wa mazingira Claudia Roth akikumbuka ziara ya mwisho ya Merkel nchini Uturuki hapo mwaka 2015, ameliambia Shirika la habari la Ujerumani dpa kwamba mkutano wa Merkel na Erdogan utatumiwa vibaya na kiongozi huyo wa Uturuki ambaye amesema utakuwa jukwaa la kukaribisha kampeni yake ya uchaguzi.Kura ya maoni inayokuja ni muhimu kwa kuufanyia mageuzi ya mfumo wa bunge.

Tishio la kufunguwa mpaka kwa wakimbizi

Polen NATO Merkel und Erdogan
Kansela Angela Merkel na Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki wakati wa Mkutano wa Kilele wa NATO nchini Poland 2016.Picha: Getty Images/S. Gallup

Kiongozi huyo wa Ururuki anatazamiwa kuishinikiza Ulaya kwa tishio la kuwafungulia mpaka wakimbizi wanaokimbilia Ulaya ambapo mkataba wa Uturuki na Ulaya umepunguza sana idadi ya wakimbizi wanaowasili Ugiriki kabla ya kuingia katika nchi nyengine za Ulaya,Uturuki imekuwa ikirudia kutishia kuufuta mkataba huo.

Msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Seibert amekanusha vikali shutuma juu ya ziara hiyo ya Merkel nchini Uturuki ambapo amesema "fikra yoyote kwamba msimamo wa Merkel utahusishwa kwa njia yoyote ile na kura ya maoni inayokuja juu ya katiba ni upuuzi."

Amesema ziara hiyo ya Merkel ni ya kikazi kwa nchi mashirika wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO na jirani muhimu wa Umoja wa Ulaya.Ameendelea kusema wakati huu ni muhimu kuzungumzia juu ya hali ya Syria na ushirikiano wa Uturuki na Umoja wa Ulaya.

Haki za binaadamu ziheshimiwe 

Türkei Mugla Verhaftungen nach Putschversuch
Kamata kamata nchini Uturuki.Picha: picture-alliance/Zuma/T. Adanali

Lakini mazungumzo ya kiserikali pekee hayatoshi anasema Marie Lucas mtaalamu wa masuala ya Utruruki katika shirika la haki za binaadamu la Amnesty International nchini Ujerumani katika mahojiano yake na DW amemtaka Merkel kudai kuheshimiwa kwa vitendo haki za binaadamu na kwamba Bibi Merkel pia azungumzie suala la kufungwa kwa wanaoikosoa seikali kwa amani na anapaswa kukutana na wapinzani na wanaharakati wa haki za binaadamu wanaokandamizwa.

Hivi karibuni imetangazwa kwamba maafisa 40 wa Uturuki wameomba kupatiwa hifadhi nchini Ujerumani baada ya jaribio la mapinduzi. Maafisa hao jeshi ambao walikuwepo katika kambi za Jumuiya ya Kujihami ya NATO wanahofia uhuru wao watakaporudi Uturuki na wengi wanahofia pia maisha yao. Waziri wa ulinzi wa Uturuki ameionya serikali ya Ujerumani kukubaliwa kwa maombi yao hayo kutakuwa na matokeo mabaya sana.

Serikali ya Ujerumani imesisitiza kwamba taratibu za kuomba hifadhi zitashughulikiwa kwa mujibu wa utaratibu wa kawaida mafanikio ya matokeo ya ziara hiyo yatakuwa muhimu kwa vyo vyote vile ni ziara nyeti kama wengi wanavyoiona.

Mwandishi: Richard Fuchs/Mohamed Dahman

Mhariri: Iddi Ssessanga