1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel akamilisha ziara ya bara la Asia

Sekione Kitojo19 Julai 2010

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amekamilisha ziara yake ya wiki moja ambapo ametia saini makubaliano kadha na maafisa wa mataifa ya bara la Asia.

https://p.dw.com/p/OOmh
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akizungumza na waandishi habari katika ziara yake nchini China.Picha: AP

Kansela  wa  Ujerumani  Angela  Merkel  amekamilisha ziara  yake  ya  wiki  moja  ambapo  ametia  saini makubaliano  kadha  na   maafisa  wa  mataifa  ya   bara  la Asia. Kansela  hata  hivyo  amekamilisha  ziara  hiyo  kwa kuzuru  Karakhstan , nchi  yenye  utajiri  mkubwa  wa mafuta, akitia  saini   makubaliano  ya  kibishara  yenye thamani  ya   zaidi  ya  euro  bilioni  2.

Ujerumani  imeanza  kujitoa  kutoka  katika   kipindi  cha kuporomoka  kwa  uchumi  na  kuingia  katika  kipindi  cha ukuaji  wa  kuridhisha  katika  miezi  michache  iliyopita kwa  mgongo  wa  mauzo  yake  ya  nje  pamoja  na kuongezeka  pia  kwa  maslahi  ya  kibiashara  nchini Urusi, China  na  hivi  sasa  Kazakhstan, hali  inayoweza kusaidia  kuimarisha  ukuaji  huo.

Makubaliano  muhimu  yaliyofikiwa  jana  Jumapili  ni mkopo  wenye  thamani  ya  euro  milioni 100  uliotolewa na  Deutsche Bank  kwa  wafanyabiashara  wadogo  na  wa kati  nchini  Kazakhstan.

Rais  wa  Kazakhstan  Nursultan  Nazarbayev ameyahimiza   makampuni  ya  Ujerumani  kujihusisha zaidi   katika  taifa  hilo, wakati  alipokutana  na  kansela Merkel. Kansela  Merkel  amedokeza   kuwa  makampuni ya  Ujerumani  yanapenda  kujishughulisha  zaidi  na masuala  ya  matumizi  ya  nishati, mawasiliano  ya  simu, ujenzi, utengenezaji  bidhaa  na  kilimo.

Ameongeza   kuwa  masharti  muhimu  kwa   kampuni  hizo kujishughulisha  zaidi  nchini  Kazakhstan ni  pamoja  na hali  jumla  ya  kuaminika  na  msingi  imara   kwa  ajili  ya kuaminiana.

Kansela  Angela  Merkel  aliondoka  katika  jimbo  la Shaanxi  asubuhi  jana  Jumapili, akikamilisha  ziara  ya siku  nne  nchini  China  ambapo  alikutana  na  viongozi wa  serikali  pamoja  na   wa  biashara  na  kutia  saini makubaliano  kuhusu  biashara, nishati  na  mazingira.

Katika  mji  mkuu  wa  jimbo  la  Xi'an , Merkel  alifuatana na  waziri  mkuu  Wen Jiabao  katika  ziara  ya  ukaguzi  wa makampuni  ya  Ujerumani  na  China, ikiwa  ni  pamoja  na miradi  ya  pamoja  inayotekelezwa  na  kampuni  la Ujerumani  la  Siemens.

Merkel  amesema   kuwa  kiwanda  hicho  cha  Siemens  ni ishara  ya  uhusiano  mzuri  baina  ya  nchi  hizo  mbili, pamoja  na  matarajio  mazuri  ya  hapo  baadaye.

Hata  hivyo, katika  mkutano  wa  hapo  kabla  wakiwa  na Merkel  na  Wen, viongozi  wa  makampuni  ya  Ujerumani na  China  walikosoa  utaratibu  wa  masoko  katika   kila nchi.

Wakati  huo  huo  kansela  wa  Ujerumani  Angela  Merkel amempoteza  mshirika  muhimu  katika  majimbo  jana Jumapili, ambapo  meya  wa  jiji  la  Hamburg  kutoka chama  chake  cha  CDU , Ole von Beust, alitangaza kujiuzulu.

Ni  waziri  mkuu  wa  sita  kutoka  chama  cha  CDU kujiuzulu  katika  muda  wa  miezi  12, na  kupunguza jumla  ya  viongozi  waandamizi  katika   chama  hicho kikubwa  nchini  Ujerumani. Pamoja  nao  ni  kujiuzulu  pia kwa  rais  wa  Ujerumani  Horst  Koehler  ambaye  alijiuzulu ghafla  Mei  mwaka  huu.

Beust  alitangaza  kujiuzulu  saa  chache   baada  ya kushindwa  vibaya  kwa  sera  zake  za  elimu  katika  jimbo la  Hamburg  ambapo  kulifanyika  kura  ya  kwanza  ya maoni juu  ya  suala  hilo.

Zaidi  ya   wapiga  kura  asilimia 54  waliikataa  sera   ya mipango  ya  serikali  ya  jimbo  hilo  kubadilisha   mfumo wa   shule  za  umma  ambapo  watoto  watatumia miaka sita  badala  ya  minne  kwa  masomo  ya  shule  za msingi.

Mwandishi : Sekione  Kitojo / DPAE

Mhariri: Josephat Charo