1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Angela Merkel ahutubia bungeni hii leo

Oumilkher Hamidou8 Septemba 2009

Serikali kuu ya Ujerumani inaliarifu bunge kuhusu kuhujumiwa malori mawili yaliyosheheni mafuta mjini Kundus

https://p.dw.com/p/JVwb
Kansela Angela Merkel ahutubia bungeni mjini BerlinPicha: picture-alliance/ dpa

Serikali kuu ya Ujerumani inaliarifu bunge kikamilifu hii leo kuhusu kisa cha mashambulio ya mabomu ya madege ya kivita ya jumuia ya kujihami ya magharibi NATO kaskazini mwa Afghanistan.Mashambulio hayo yaliyoamriwa na kanali wa kijerumani,yamekosolewa ndani na nje ya Afghanistan.

Kansela Angela Merkel amelihutubia bunge hii leo kuhusiana na kadhia hiyo.Na waziri wa mambo ya nchi za nje Frank-Walter Steienmeier amebidi pia kujibu masuala ya wabunge kuhusiana na kisa hicho kilichopelekea waziri wa ulinzi Franz Josef Jung kulaumiwa na kila upande humu nchini.

"Kadhia hii lazma ifafanuliwe" amesema kansela Angela Merkel katika kipindi cha "Wahlarena" au uwanja wa uchaguzi" cha kituo cha televisheni cha ARD jana usiku.Wakati huo huo kansela amehimiza hali iimarike nchini Afghanistan hadi kufikia mwaka 2014.

Kansela Angela Merkel ameendelea kusema:

"Tunabidi tuhakikishe maendeleo yanapatikana katika kipindi cha miaka mitano ijayo na nnaamini,jambo hilo linawezekana ikiwa sote tutafanya bidii."

Walinzi wa mazingira wamemtaka kansela Angela Merkel aombe radhi kwa wahanga wa shambnulio hilo la mabomu.

Waziri wa ulinzi Franz Josef Jung anautetea uamuzi wa kuhujumiwa malori mawili yaliyokua yamesheheni mafuta .

Akizungumza kupitia kituo cha televisheni cha ARD jana usiku,waziri wa ulinzi Josef Jung amesema tunanukuu:"Wataliban walisema hivi karibuni wanapanga kufanya shambulio kama hilo kabla ya uchaguzi mkuu nchini Ujerumani."Mwisho wa kumnukuu.

Bundeswehr in Kundus Afghanistan nach Anschlag
Mwanajeshi wa Ujerumani apiga doria KundusPicha: AP

Lawama za rais Hamid Karzai kwa jeshi la shirikisho Bundeswehr zimepingwa na vyama ndugu vya CDU/CSU.

Kwa mujibu wa kituo cha pili cha televisheni ZDF,ripoti ya awali ya utafiti uliosimamiwa na jumuia ya kujihami ya magharibi NATO imeonyesha mashambulio dhidi ya malori mawili ya mafuta yaliyokua yametekwa nyara na wataliban huko Kundus yamegharimu maisha ya watu kati ya 70 na 78.Ripoti za vyombo vya habari zilizungumzia juu ya wahanga wasiopungua 130.

Mbunge wa ulaya Elmar Brok wa kutoka chama cha CDU ameshauri shughuli za vikosi vya kimataifa nchini Afghanistan zimalizike haraka."Tunahitaji mkakati wa kuaminika wa kujitoa Afghanistan-kwa sharti lakini nchi hiyo inajikuta katika hali ya kudhamini wenyewe usalama na nidhamu."Amesema mwanachama huyo wa kamati ya bunge la ulaya inayoshughulikia masuala ya nchi za nje.

Nchini Afghanistan kwenyewe gari moja limeripuliwa mjini Kaboul na kugharimu maisha ya raia watatu.Raia sita wengine wamejeruhiwa.Wanajeshi watatu wa kimarekani na mmoja wa Ubeligiji wamejeruhiwa pia.Shambulio hilo lilikua limelengwa vikosi vya jumuia ya kujihami ya magharibi NATO katika mji mkuu huo wa Afghanistan.

Hili ni shambulio la pili baada ya lile la jana usiku ambapo waasi walihujumu kambi ya kijeshi ya kimarekani Camp Phenix karibu na Kaboul.

Msemaji wa waasi wa taliban ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP wanahusika na mashambulio hilo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/DPA

Mhariri:Othman Miraji