1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Angela Merkel ahimiza makubaliano ya ushirikiano mpya kati ya Umoja wa Ulaya na Urusi.

Mohamed Dahman5 Juni 2008

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ahimiza kufikiwa kwa makubaliano mapya ya ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na Urusi kufuatia mazungumzo yake na Rais mpya wa Urusi Dmitry Medvedev ambaye yuko ziarani Ujerumani.

https://p.dw.com/p/EENF
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Dmitry Medvedev wakizungumza na waadishi wa habari baada ya kukutana mjini Berlin.Picha: AP

Merkel amekaririwa akisema kufuatia mazungumzo yake na Medvedev katika ziara yake ya kwanza barani Ulaya tokea ashike wadhifa huo kutoka kwa Vladimir Putin mwezi uliopita kwamba anazungumza kwa kupendelea kumalizika kwa haraka mazungumzo ya kufikia makubaliano ya ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na Urusi.

Umoja wa Ulaya na Urusi zinatazamiwa kuanza mazungumzo hayo yaliochelewa kwa muda mrefu katika mkutano wa viongozi uliopangwa kufanyika huko Siberia baadae mwezi huu ambapo uhusiano wa nishati litakuwa suala la juu katika agenda wakati Umoja wa Ulaya ukizidi kuwa tegemezi kwa mafuta na gesi ya Urusi.

Merkel pia ametowa wito wa kufanyika kwa mikutano ya mara kwa mara kati ya Urusi na Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi NATO.

Merkel na kiongozi huyo wa Urusi pia wamesema kwamba wanakusudia kuondowa upinzani wa majirani zao wanaopinga kujengwa kwa bomba la mafuta chini ya bahari ya Baltik kusafirisha gesi ya Urusi moja kwa moja hadi Ujerumani.

Merkel amesisitiza kwamba bomba hilo halikusudii kumdhuru mtu yoyote yule hususan Poland ambayo imeelezea wasi wasi wake wa kupita kwa bomba hilo kwa kuhofia mustakbali wa usalama wake wa nishati.

Medvedev amesema bomba hilo ambalo shirika la Gazprom la Urusi lina udhibiti wa asilimia 51 litarahisisha usambazaji wa gesi kwa bara zima la Ulaya.

Medvedev ambaye ni mwenyekiti wa zamani wa Gazprom amesema bomba hilo litaanza kutowa gesi ifikapo mwaka 2011.

Mazungumzo juu ya makubaliano mapya ya ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na Urusi huko Siberia mwishoni mwa mwezi huu yanafanyika baada ya Poland na Lithuania kuondowa upinzani wao.

Viongozi hao wawili pia wamejadili mfumo wa sheria nchini Urusi ambapo Medvedev amekiri kwamba una mapungufu kwa kusema kwamba mfumo wao huo wa sheria uko katika awamu ya maendeleo na kusisitiza kwamba mageuzi ni jukumu muhimu.

Hotuba ya Medvedev juu ya sera ya kigeni katika Kikao cha Ujerumani na Urusi baadae leo hii ambapo atazungumzia masuala makuu ya kimataifa kwa mara ya kwanza tokea ashike madaraka inasubiriwa kwa hamu kuonyesha dalili iwapo yumkini akafuata mkondo usio wa malumbano sana kama ule wa mtangulizi wake Putin.

Mbali na mzunagumzo yake na Merkel na Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter- Steinmeir kiongozi huyo wa Urusi pia atakutana na Rais Hörst Kohler wakati wa ziara yake hiyo fupi ya masaa manane nchini Ujerumani.