1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

GM Opel

Josephat Nyiro Charo27 Agosti 2009

Mustakabal wa kampuni ya Opel haujulikani

https://p.dw.com/p/JHS9
Nembo ya kampuni ya OpelPicha: AP

Mustakabal wa kampuni ya kutengeneza magari ya Opel hapa Ujerumani haujajulikana. Mpaka sasa haijabainika wazi vipi kampuni hiyo inavyotakiwa kujikwamua kutokana na mgogoro wa kiuchumi. Baraza la viongozi wa kampuni ya General Motors, inayoimiliki kampuni ya Opel, mpaka sasa halitaki kuridhia kampuni hiyo ichukuliwe na kampuni ya kutengeneza vipuri vya magari ya Magna ambayo inaungwa mkono na serikali ya Ujerumani, kuinunua kampuni hiyo ya Opel.

Kutofikia uamuzi pia ni aina fulani ya uamuzi. Hatima ya kampuni ya Opel bado inayumba, inaendelea kuelea katika anga, haijulikani. Kwa sababu serikali ya Ujerumani pamoja na mawaziri wakuu wa majimbo matatu ya Ujeruamni kunakopatikana viwanda vya kampuni ya Opel wanaendelea kuvutana, kampuni ya General Motors, inacheza mchezo wa poka. Baada ya kampuni ya General Motors nchini Marekani kufaulu kujikwamua kutokana na kufilisika katika kipindi kifupi, meneja wa kampuni hiyo mjini Detroit anachukua muda mrefu kuamua kuhusu mustakabal wa biashara ya kampuni hiyo barani Ulaya na hivyo kuendeleza kitendawili cha kampuni ya Opel ya Ujerumani.

Kwa sababu hiyo, shinikizo kuhusu wakati linazidi kuongezeka kwa mara nyingine tena kwani kiasi cha euro bilioni 1,5 kutoka kwa walipa-kodi wa Ujerumani ambazo zilinuiwa kuinusuru kampuni ya Opel isifilisike, kitaisha muda mfupi kabla mwaka huu kumalizika. Juu ya hilo, mpango maalum wa serikali wa kubadilisha magari ya zamani ambao umeimarisha biashara ya kampuni ya Opel, utamalizika katika wiki chache zijazo.

Kampuni ya Opel itakabiliwa na wakati mgumu zaidi kwani licha ya manufaa iliyopata kutokana na mpango maalum wa serikali ya Ujerumani wa kubadilisha magari ya zamani, kampuni hiyo pia ilikuwa ikipata hasara ya mamilioni ya euro. Hivi karibuni serikali kuu ya Ujerumani mjini Berlin pamoja na serikali za mikoa mitatu kuliko na viwanda vya kampuni ya Opel, zitakabiliwa na chaguo; Kuiacha kampuni ya Opel ifilisike au zitafute mpango mpya wa kuisaidia kifedha kampuni hiyo.

Pia inaonekana Wamarekani hawana nia ya kuiuza kampuni ya Opel kwa kampuni ya kutengeneza vipuri ya Canada, Magna, benki ya Urusi ya Sberbank wala kampuni ya magari ya Urusi GAZ. Kwani kwa njia hiyo kampuni ya General Motors itakuwa na shughuli chache za kibiashara katika soko la Ulaya kupitia kiwango kidogo cha hisa katika kampuni ya Opel.

Kampuni ya General Motors inajiona kuwa kampuni kubwa ya kimataifa na inataka iendeleze biashara yake barani Ulaya. Ndio maana inapendelea kampuni ya uwekezaji fedha ya RHJ inunue hisa nyingi za kampuni ya Opel, iifanyie mageuzi halafu iiuze tena kwa kampuni ya General Motors.

Kampuni ya General Motors inacheza mchezo wa paka na panya kuvuta muda, hali inayoiweka serikali ya Ujerumani na serikali za mikoa ambako kuna viwanda vya kampuni ya Opel chini ya shinikizo kubwa. Wakati huo huo ni jaribio la kuzuia uamuzi muhimu kuhusu mustakabal wa kampuni ya Opel kupitishwa wakati wa uchaguzi mkuu hapa nchini. Hiyo ina maana katika miezi ijayo baada ya uchaguzi kufanyika kampuni ya General Motors inataka kueleza kwa kina nini kitakachotokea kwa kampuni ya Opel.

Mwandishi:Karl Zawadzky/ZR/Josephat Charo

Mhariri:Abdul-Rahman