1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampuni ya General Motors kusaidiwa isifilisike

Charo Josephat/ RTRE1 Juni 2009

Uuzaji wa kampuni ya Chrysler wakamilika

https://p.dw.com/p/I1NU
Makao makuu ya kampuni ya General Motors mjini DetroitPicha: AP

Kampuni ya kutengeneza magari ya Marekani General Motors itawasilisha ombi kusaidiwa kuondokana na kitisho cha kuwa muflis hii leo mjini New York. Rais wa Marekani Barack Obama anatarajiwa baadaye leo kuzungumzia kuhusu sekta ya magari. Huku ikiwa imekabiliwa na hali ngumu kutokana na kunywea kwa uchumi wa Marekani, kampuni ya General Motors imeachwa bila chaguo lingine kwani tarehe ya mwisho iliyowekewa na serikali kufanya mageuzi ikimalizika leo.

Kampuni ya General Motors yenye makao yake huko mjini Detroit katika jimbo la Michigan itakuwa kampuni ya kwanza kubwa ya kutengeneza magari kuwahi kuwasilisha ombi la kusaidiwa isifilisike katika historia ya Marekani. Kampuni hiyo hata hivyo inatarajiwa kuwasilisha stakabadhi zake mwendo wa saa mbili kamili leo asubuhi saa za New York kuanza mchakato wa mahakama huku ikisaidiwa na serikali ya Marekani, chama chake kikubwa cha wafanyakazi na idadi kubwa ya wakopeshaji wake. Rais Obama na mkurugenzi wa kampuni ya General Motors, Fritz Henderson watazungumzia kuhusu mwelekeo mpya wa kampuni hiyo baadaye leo na kusisitiza umuhimu wa kuisadia kwa matumaini kwamba hiyo ndiyo njia pekee ya kuikoa kutokana na kuwa muflis.

USA Wahlen Demokraten Barack Obama zu seinem Pastor
Rais wa Marekani Barack ObamaPicha: AP

Hatua ya kampuni ya General Motors inaifungulia mlango serikali ya Marekani kumiliki asilimia 60 ya hisa za kampuni hiyo kwa mabadilishano ya mkopo wa dola bilioni 30 kutoka kwa serikali juu ya dola bilioni 19.4 ilizopokea hapo awali kugharamia hasara na shughuli zake. Kwa mujibu wa maafisa wa ngazi ya juu waliozungumzia mipango hiyo hapo jana, utawala wa rais Obama unaamini kampuni ya General Motors inaweza kumaliza mchakato wa mahakama katika kipindi cha miezi miwili hadi mitatu kama kampuni ndogo na isiyo na deni.

Ikulu ya Marekani imesema leo itakuwa siku nyingine ya kihitoria kwa kampuni ya General Motors yenye umri wa karne moja, inayoashiria mwisho wa kampuni ya General Motors iliyozeeka, lakini mwanzo wa enzi mpya. Kampuni hiyo inapania kutumia mahakama kulipa deni lake la dola bilioni 27 na kuuza mali zake bora kwa kampuni mpya, na kuachana na utengenezaji wa aina nne za magari yake zikiwemo Pontiac, Saab, Saturn na Hummer. Kampuni hiyo itafunga matawi yake ya uchuuzi huko Amerika Kaskazini na kupunguza nafasi zaidi ya 30,000 za ajira.

Wachuuzi, wasambazaji na biashara nyengine kubwa na ndogo zinazohusina moja kwa moja katika sekta ya magari zitaathirika. Takriban wafanyakazi 500,000 waliostaafu kutoka kwa kampuni ya General Motors pamoja na wengine zaidi ya 150,000 ya jamaa zao wanaitegemea kampuni hiyo kwa bima ya afya na malipo ya uzeeni. Wastaafu watapunguziwa bima zao za afya ingawa mipango ya malipo ya uzeeni haitarajiwi kuathirika.

Matawi ya General Motors barani Ulaya, Vauxhall na Opel, yako katika mchakato wa kuuziwa kampuni ya kutengeneza vipuri ya Canada na Austia, Magna, kwa msaada wa serikali ya Ujerumani. Kampuni mpya ya General Motors itasimamiwa na serikali mpaka itakapoweza kujitosheleza bila msaada wa serikali. Ikulu ya white house itasaidia kuwateua wakurugenzi wapya wa bodi ya kampuni hiyo, lakini maafisa wamesema serikali haina nia ya kujiingiza katika uendeshaji wa shughuli za kila siku katika kampuni ya General Motors.

Kampuni ya General Motors inafuata mkondo wa kampuni ya Chrysler, hasimu wake mdogo kibiashara, ambayo ililazimika kukabiliwa na muflis mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu. Kampuni ya Chrysler inatarajiwa kuondoka mahakamani mwezi Juni ikiwa nzima, lakini ikisimamiwa kikamilifu na kampuni ya kutengeneza magari ya Italia, Fiat. Serikali ya Marekani mjini Washington imesema kampuni ya General Motors inatakiwa kuiga mfano wa kampuni ya Chrysler.