1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampuni ya AgriSol yatuhumiwa kuwapokonya ardhi maelfu ya wakimbizi Tanzania

13 Julai 2012

Kampuni ya Kimarekani, AgriSol Energy, inatuhumiwa kupokonya ardhi Tanzania na inakadiriwa kuwa zaidi ya wakimbizi 160,000 wenye asili ya Kirundi waliokuwa wakiishi katika maeneo hayo kwa miongo kadhaa wameadhirika.

https://p.dw.com/p/15X5e
Wakulima nchini Burundi kazini
Wakulima nchini Burundi kaziniPicha: picture-alliance/Ton Koene

Kampuni moja kubwa ya nishati ya Kimarekani, AgriSol Energy, inatuhumiwa kwa kupokonya ardhi nchini Tanzania na inakadiriwa kuwa zaidi ya wakimbizi 160,000 wenye asili ya Kirundi waliokuwa wakiishi katika maeneo hayo kwa miongo kadhaa wataathirika na kadhia hiyo.

Pendo Paul na taarifa zaidi

Kwa mujibu waTaasisi ya Oakland, inayoshughulikia masuala ya mazingira, kuna malalamiko ya kimaadili yaliyoripotiwa na wakazi wa Iowa kwamba Kampuni hiyo ya AgriSol inapata faida kwa kuwanyang'anya kinguvu ardhi wakimbizi hao, ambao wengi wao ni wakulima wadogo wadogo, na kukodishwa ardhi hiyo na serikali ya Tanzania kwa senti 25 kwa heka moja, ardhi yote hiyo bila kulipa kodi ya aina yoyote ile.

Mradi huo unaweza ukaipatia kampuni hiyo, ambayo imeanzishwa na Bruce Rastetter, dola milioni 300 kwa mwaka.

Akielezea masikitiko yake, aliyekuwa mfugaji mmoja wa nguruwe kutoka mjini Rhodes, Larry Ginter, amesema amesikitishwa na uonevu huo unaofanywa dhidi ya wakulima hao nchini Tanzania.

Ginter anaongeza kusema kwamba mchezo huo unaofanywa na Agrisol umeanza siku nyingi na anavyoona yeye huo ni ukoloni wa kisasa, ambao ameuita ni wizi wa hali ya juu.

Hata hivyo, msemaji wa AgriSol nchini Tanzania amekanusha tuhuma hizo na kudai kuwa ni serikali ya Tanzania yenyewe ndio iliyoasisi makubaliano hayo ya kuwaondoa wakimbizi hao zaidi ya laki moja na sitini.

Akitoa utetezi huo, Mkurugenzi wa Mawasiliano nchini Tanzania, Henry Akona, amesema si sahihi kuinyooshea kidole Kampuni ya Agrisol katika sakata hilo.

Katika tovuti ya kampuni hiyo, kuna taarifa inayodai kwamba mradi huo umechelewa kuanza huko Katumba na Mishamo kutokana na malalamiko hayo. Na mradi huo utaendelea tu pale madai hayo yatakapotafutiwa ufumbuzi.

Jinsi Tanzania inavyohusika

Mradi wa AgriSol uliungwa mkono na serikali ya Tanzania ili kwenda sambamba na Kilimo Kwanza, mkakati uliozinduliwa mwaka 2009 na Baraza la Kitaifa la Biashara TNBC, ukiwa na lengo la kuimarisha maendeleo ya kilimo kupitia ushirikiano na sekta ya umma na binafsi.

Katika ushirikiano huo, ArgiSol itasaidiwa katika kupewa ardhi ya kilimo cha kibishara kitakachohusisha mazao ya chakula kama vile mahindi na soya pamoja na ufugaji wa kuku.

Ili kutekeleza hilo, kampuni hiyo ya Kimarekani imejiandaa kuzindua uwekezaji wenye thamani ya dola milioni 100 nchini Tanzania katika kipindi cha miaka 10 ijayo.

Lengo kuu la AgriSol linasemekana ni kusaidia kuimarisha ugavi wa chakula cha ndani ya nchi, kutoa fursa za ajira na uchumi kwa wananchi wa Tanzania na hivyo kuchochea uwekezaji katika kuimarisha miundombinu ya nchi hiyo.

Kwa upande wake Anuradha Mittal, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Oakland, ambaye amefanya utafiti nchini Tanzania, amesema sera hizo zinazuia biashara ya ndani kwani wenyeji hao wameambiwa kuwa hawataanzisha biashara mpya. Mittal ameongeza kusema kwamba wakimbizi hao hawana chao isipokuwa kuhama makazi hayo.

Kwa mujibu wa hati ya makubaliano iliyoandikwa na Iddi Simba kwa niaba ya AgriSol, serikali ya Tanzania iliionyesha kampuni hiyo maeneo matatu ya ardhi magharibi mwa nchi hiyo, ambayo awali yalikuwa ni makambi ya wakimbizi ambayo yalitakiwa kufungwa katika siku za usoni.

Hata hivyo, Simba hakuwa serikalini wakati wa kuandikwa kwa makubaliano hayo. Alilazimishwa kujiuzulu mwaka 2001 katika ngazi ya uwaziri wa biashara, baada ya kugundulika kuwa alitoa vibali haramu vya kuingiza sukari nchini Tanzania.

Na Kampuni ya AgriSol imetamka wazi kuwa imeachana na mpamgo wa kuwekeza katika maeneo ya Katumba na Mishamo. Kwa sasa, inalenga kuwekeza katika miji ya Kigoma, Lugufu na Basanza.

Mwandishi: Ndovie, Pendo Paul\IPS

Mhariri: Josephat Charo