1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kambi za waasi zashambuliwa Mali

Admin.WagnerD4 Februari 2013

Jeshi la Ufaransa nchini Mali sasa linaripotiwa kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya maghala ya mafuta na kambi za vikundi vya Waislamu wenye msimamo mkali huko kaskazini mwa Mali.

https://p.dw.com/p/17XXs
Ndege ya kivita Mali
Ndege ya kivita MaliPicha: picture-alliance/dpa

Akizungumza kupitia radio moja ya Kifaransa, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Laurent Fabius, amesema usiku kucha kuamkia leo ndege za kivita zimeshambulia mkoa wa Kidal, uliyopo mpakani mwa Mali na Algeria. Amesema hatua hiyo ni moja kati ya malengo makubwa ya kuweza kukata uwezo wa kujipatia mahitaji yao muhimu kwa kundi hilo ambalo lilidhibiti sehemu kubwa ya eneo hilo na kushinikiza sheria kali kwa wakazi wa maeneo hayo.

Aidha Fabius amesema kwa mashambulizi hayo waasi hao hawawezi kuendelea kudumu kuishi kwa muda mrefu katika eneo hilo, labda wawe na hazina mpya ya mahitaji yao. Ufaransa iliingia nchini Mali, Januari 11 kwa lengo la kuwazuia kusonga mbele kundi la waasi la Ansar Dine lenye mafungamano na al-Qaida.

Fabius amerejelea msimamo wa nchi yake wa kutaka jeshi la Afrika kuchukua haraka kwa kadri iwezekanavyo dhamana ya ulinzi katika mji wa kihistoria wa Timbuktu. Kwa sasa, Ufaransa inadhibiti mji huo na mingine kadhaa tangu ianze operesheni hiyo.

French special forces drive through the city of Gao, Northern Mali, Wednesday Jan. 30, 2013. Islamist extremists fled the city Saturday after French, Chadian and Nigerien troops arrived, ending 10 months of radical islamic control over the city.(Foto:Jerome Delay/AP/dapd)
Vikosi vya Mali na Ufaransa mjini GaoPicha: dapd

OIC kuzungumzia ghasia za Mali

Wakati mapigano yakiendelea nchini Mali, viongozi wa Jumuiya ya Mataifa ya Kiislamu, OIC, wanatarajiwa kukutana mjini Cairo, Misri, ambako pamoja na mgogoro wa Syria, suala la Mali litapewa nafasi. Taarifa zinaeleza kuwa mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa hayo wanaanza kikao cha maandalizi leo hii. Mkutano huu mkubwa utawakutanisha viongozi 26 kati ya mataifa 57 ya OIC.

Rais Mohamed Morsi wa Misri safari hii anatarajiwa kuchukua uongozi wa umoja huo ambao kwa kawaida nafasi yake inatolewa kwa zamu kwa nchi wanachama. Katibu Mkuu wa OIC, Ekmeleddin Ihsanoglu, amesema mkutano huu wa sasa ulipaswa kufanyika mwaka 2011 lakini uliaharishwa baada ya kutokea vuguvugu la mageuzi katika mataifa ya Kiarabu na kuwaondoa watawala wanne wa kiimla akiwemo Hosni Mubarak wa Misri.

Islamic countries' leaders pose for official photos before an extraordinary session of the Organization of Islamic Conference in Mecca, Saudi Arabia, Tuesday, Aug. 14, 2012. Saudi Arabia’s King Abdullah hosted the conference, a body of 57 member states, which agreed to discuss suspending Syria’s membership. (Foto:AP/dapd)
Viongozi wa OIC walipokutana mjini MakkaPicha: AP

Mwanadiplomasia huyo wa zamani ya Kituruki amesema mkutano huo wa kilele utajadili migogoro mikubwa katika mataifa ya Kiislamu. Aidha ameonesha kusikitishwa kwake na migogoro sambamba na kasi ya vikundi vyenye misimamo mikali ya Kiislamu ukiwemo huu unaofukuta sasa wa Mali. Tofauti za sera za mambo ya nje na kusaidiana kwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo, ni miongoni mwa mambo yatakayojadiliwa katika mkutano huo wa kilele wa siku mbili.

Mwandishi: Sudi Mnette/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef