1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kagawa, Okazaki waichangamsha Bundesliga

15 Septemba 2014

Bundesliga, mwishoni mwa wiki ilimilikiwa na Japan baada ya Shinji Kagawa kuonyesha umahiri wake tangu alipojiunga na klabu yake ya zamani Borussia Dortmund naye Shinji Okazaki akaifungia Mainz mabao mawili.

https://p.dw.com/p/1DCWM
Fußball Bundesliga 3. Spieltag Borussia Dortmund vs. SC Freiburg
Picha: Getty Images/J. Schwarz

Kagawa alirejea baada ya kuwa na kipindi kigumu cha miaka miwili katika klabu ya Manchester United na hakuchelewa kudhihirisha kurejea kwake, alipofunga goli moja na kuandaa jingine wakati BVB wakiibwaga Freburg magoli matatu kwa moja.

Kocha Jurgen Klopp hakuchelewa kummiminia sifa Mjapan huyo ambaye bila shaka atakuwa muhimu kwa vijana hao wa njano. Mjapan mwingine Shinji Okazaki, alifunga mabao mawili na kuisaidia Mainz kushinda Hertha Berlin magoli matatu kwa moja.

Kwingineko, jana, Hanover waliwanyamazisha Hamburg magoli mawili kwa bila matokeo ambayo yalimwongezea mbinyo kocha wao wa zamani Mirko Slomka baada ya kuwa na mwanzo mbaya wa msimu na Hamburg. Slomka amesema baada ya mechi kuwa wataendelea kutia bidii ili kuyaweka mambo sawa. "kwa kuanza, nadhani timu imeonyesha ari na mchezo mzuri. Nadhani pia kuwa tulitamba sana na tungestahili kupat goli. Lakini lengo letu kuu ni kuwa lazima tutie bidii sana msimu huu. Hicho ndio tunachokosa kwa sasa. Yaani hisia ya mafanikio, katika mapambano mengi, na katika mashambulizi ya langoni, Hanover leo walikuwa mbele yetu".

Shinji Okazaki aliwafurahisha mashabiki kwa kuifungia Mainz magoli mawili
Shinji Okazaki (kulia) aliwafurahisha mashabiki kwa kuifungia Mainz magoli mawiliPicha: Getty Images/M. Kern

Hapo awali, Augsburg walipata ushindi wao wa kwanza msimu huu kwa kuwafunga Eintracht Frankfurt goli moja kwa sifuri. Tobias Werner ni mchezaji wa Augbsurg akizungumza baada ya mechi hiyo ngumu. "Bila shaka sote hatujaridhika na mwanzo wetu wa msimu. Hasa kubanduliwa nje ya Kombe la Shirikisho la Soka Ujerumani – DFB.

Lakini tumekuwa watulivu na unaona kile tumekifanya kikosini, tungefanya mambo kuwa rahisi zaidi, hasa nafasi niliyokosa kufunga, lakini ndio hali y ampira. Tuna furaha tumeponyoka na pointi tatu".

Mario Götze na Franck Ribery waliipa Bayern Munich ushindi wa magoli mawili kwa sifuri dhidi ya STUTTGART. Mmshambuliaji wa Borussia Moenchengladbach Max Kruse aliiongoza timu yake kuibambua Schalke magoli manne kwa moja. Ralf Fährmann ni mlinda lango wa Schalke. "Hatungeweza kutekeleza kile tulitarajia na kwa kweli hatukupambana vizuri. Tumeipa nafasi nyingi sana ya kutamba nyumbani timu yenye uwezo mkubwa kama Gladbach".

Wolfsburg walitoka sare ya goli moja kwa moja na Hoffenheim, huku pia timu mbili zilizopandishwa daraja msimu huu Paderborn na Cologne zikitoka sare ya kutofungana bao.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Yusuf Saumu