1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jukwaa la usalama wa taifa Marekani

8 Septemba 2016

Donald Trump na Hilary Clinton Jumatano (07.09.2016) kila mmoja ameumbuwa udhaifu wa mwenzake katika jukwaa kuhusu usalama wa taifa lilionyeshwa moja kwa moja na televisheni nchini Marekani.

https://p.dw.com/p/1JyHF
Picha: Reuters/M. Segar//Getty Images/AFP/B. Smialowski

Katika jukwaa hilo kuhusu usalama wa taifa lilifonyika New York Marekani akijibu suali Trump amesema rais wa Urusi Vladimir Putin ni kiongozi mzuri kuliko hata Rais Obama wa Marekani.

Amesema "Iwapo atanisifu nami nitamsifu tayari nimesema kwamba ni kiongozi mzuri. Mwanaume huyo ana udhibiti mzuri sana kwa nchi yake:Mfumo wao utawala ni tafauti sana siupendi sana lakini ni jambo la uhakika chini ya mfumo amekuwa kiongozi mzuri kuliko hata rais wetu.Tuna nchi iliogawika.Tuna nchi ambapo una Hilary Clinton na baruwa pepe zake ambazo hakuna mtu aliyeziona, amezifuta baruwa pepe 33,000 baada ya kuitwa na bunge la Marekani.Iwapo utafanya jambo hilo katika shughuli za kibinasi utatupwa gerezani."

Amemsifu kiongozi huyo wa Urusi ambaye amesema anaungwa mkono na wananchi wake kwa asilimia 82 na kwamba anafikiri atakuwa na uhusiano mzuri sana naye.

Wagombea wa urais wa Marekani Donald Trump wa chama cha Republikan na Hilary Clinton wa Chama cha Demokratik kila mmoja alitumia dakika 30 kujibu masuali mbali mbali lakini hawakuwako jukwaani kwa pamoja jukwaa hilo limetumika kama chachu kuelekea kwenye midahalo inayosubiriwa kwa hamu itakayowakutanisha ana kwa ana wagombea hao wa urais

Baruwa pepe zamwandama Clinton

Clinton alikuwa wa kwanza kupanda jukwaani na haraka alijikuta akijibu maswali mengi kuhusu muda wake aliokuwa serikalini. Amekiri kwamba amefanya makosa katika kutegemea baruwa pepe zake binafsi na kumpyuta yake binafsi wakati akiwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani na kwa kupiga kura ya kuunga mkono uvamizi wa Iraq wakati akiwa seneta hapo mwaka 2003.

Masanamu yaliyomithilishwa na sura za Clinton na Trump.
Masanamu yaliyomithilishwa na sura za Clinton na Trump.Picha: DW/F. Steiner

Lakini ametetea uamuzi wake wa kuunga mkono Marekani kuingilia kijeshi Libya kusaidia kumn'gowa dikteta Muammar Gaddafi licha ya machafuko yaliyofuatia baadae.Alionekana kukasirika mara nyengine wakati suala la mamamuzi yake ya zamani linapoibuliwa mara kwa mara.

Clinton amesema "Vitu vya siri huwa vinawekewa anwani ambayo husema siri kubwa ....ni siri. Hakuna kitu hicho na nitarudia kusema na hilo limeyakinishwa na repoti ya Idara ya Sheria kwamba hakuna baruwa pepe hata moja ambayo niliyotumiwa au niliyopokea yenye anwani hiyo."

Clinton ameomba ahukumiwe kwa mujibu wa rekodi yake.Ikiwa imebakia miezi miwili tu kabla ya Siku ya Uchaguzi suala la usalama wa taifa limekuwa nguzo kuu ya Ikulu ya Marekani.

Wagombea wote wawili wanaamini wana turufu huku Clinton akijigamba kwa tajiriba yake kwa kulinganisha tafauti na Trump ambaye hatabiriki na ambaye chama cha Tepublikana kinasema mashaka ya Wamarekani kuhusu usalama yataachwa pale pale iwapo watamchaguwa Clinton waziri wa mambo ya nje wa zamani wa utawala wa Obama.

Mwandishi : Mohamed Dahman /AP/Reuters

Mhariri:Yusuf Saumu