1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jukwaa la kiuchumi kuhusu nishati na hali ya hewa kuanza leo

Kabogo Grace Patricia20 Septemba 2010

Jukwaa hilo linalofanyika mjini New York, Marekani lina lengo la kutatua masuala yaliyosababisha kukwama kwa mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa uliofanyika mwaka uliopita.

https://p.dw.com/p/PHdu
Makao makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani.Picha: AP

Viongozi wa mataifa 17 yenye jukumu la kupunguza kwa asilimia 80 viwango vya gesi vinavyochafua mazingira na vinavyolaumiwa kwa kusababisha hali ya ujoto duniani wanakutana kujaribu kuondoa vizingiti vilivyokwamisha mazungumzo ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa, lakini wachambuzi wanasema kuna matarajio madogo ya kupatikana kwa maendeleo katika mkutano huo.

Jukwaa hilo kuu la kiuchumi kuhusu nishati na hali ya hewa linaloanza hii leo mjini New York, Marekani litawajumuisha maafisa wa ngazi za juu wa serikali, akiwemo mjumbe wa Marekani kwa ajili ya mabadiliko ya hali ya hewa, Todd Stern. Rais Barack Obama alianzisha mikutano hiyo ili kuyawezesha mazungumzo ya hali ya hewa kutokana na kushindwa vibaya kwa mkutano wa Umoja wa Mataifa uliofanyika mwaka uliopita mjini Copenhagen. Mkutano mwingine wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa umepangwa kufanyika Cancun, Mexico Novemba mwaka huu.

Matarajio ya mkutano huo

Mchambuzi katika baraza la Mahusiano ya Kigeni, Michael Levi anasema kuwa hadhani kama kuna mtu yoyote anatarajia kutolewa taarifa kuu. Bwana Levi ameliambia shirika la habari la AFP kuwa huo ni mkutano wa kikazi kwa sababu wahusika wengi wakuu wako katika mji huo huo kwa wakati huo huo lakini wakihudhuria mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Mchambuzi huyo anasema wajumbe hawatatafuta njia kali za kutatua mjadala wa mabadiliko ya hali ya hewa, bali kutafuta njia za kuelezea masuala, wakikiri kuwa kuwa uwezekano mwingine wa kukwama kwa mkutano wa Cancun.

Mwanamazingira, Bill Mekibben anasema kutokana na bunge la Marekani kushindwa kupitisha sheria ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa imelifanya suala hilo kuwa gumu zaidi katika kuchukua hatua madhubuti za kufikia makubaliano imara huko Cancun. Mwezi Juni Bunge la Marekani lilipitisha muswada utakaoanzisha kwa mara ya kwanza kabisa mfumo wa biashara inayozuia kupunguza matumizi ya gesi inayochafua mazingira ambayo inalaumiwa pia kwa kuongeza hali ya ujoto duniani na kuruhusu biashara kwa njia ya mikopo. Mekibben anasema kuwa hatua zaidi za kimataifa zinahitajika kwa ajili ya kuanzisha shinikizo la kuunga mkono suala la kupunguza matumizi ya gesi inayochafua mazingira.

Mikutano mingine

Mbali na mkutano huo wa siku mbili unaoanza hii leo, baadaye mwezi huu Mawaziri wa Mazingira wa nchi 45 wanatarajiwa kukutana huko Geneva kufuatia mwaliko uliotolewa na serikali za Uswisi na Mexico. Pia wachambuzi kutoka mataifa 194 yaliyosaini mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa watakutana Tianjin, China mwezi ujao wa Oktoba kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mazungumzo hayo. Mazungumzo ya wiki ijayo yatawajumuisha wawakilishi kutoka Australia, Brazil, Uingereza, Canada, China, Umoja wa Ulaya na Ufaransa. Wengine watatoka Ujerumani, India, Indonesia, Italia, Japan, Mexico, Urusi, Afrika Kusini, Korea Kusini na Marekani.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)

Mhariri:Abdul-Rahman