Juhudi za upatanishi Côte d′Ivoire zashika kasi | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 04.01.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Juhudi za upatanishi Côte d'Ivoire zashika kasi

Wapatanishi wa ECOWAS na AU waondoka mikono mitupu mjini Abdijan na sasa wanakutana na Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria mjini Abuja, kuripoti matokeo ya mkutano wao na Laurent Gbagbo.

Laurent Gbagbo, Rais anayesemekana kuwa alishindwa kwenye uchaguzi wa Côte d'Ivoire

Laurent Gbagbo, Rais anayesemekana kuwa alishindwa kwenye uchaguzi wa Côte d'Ivoire

Wapatanishi wa Jumuia ya Uchumi ya Afrika ya Magharibi (ECOWAS) na Umoja wa Afrika (AU) wameondoka Abidjan; jana usiku (3 Januari 2011), bila ya dalili ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Côte d'Ivoire. Bado, vuta n'kuvute inaendelea katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga na marais Boni Yayi wa Benin, Ernest Koroma wa Sierra Leone, na Pedro Pires wa Visiwa vya Cape Verde walijaribu siku nzima jana kuupatia ufumbuzi mgogoro uliosababishwa na uchaguzi wa Novemba 28 mwaka jana, na uliogharimu maisha ya watu karibu 200.

Lakini baada ya kuonana mara mbili na Laurent Gbagbo na kuzungumza na Alassane Outtara, Raila odinga ambae ni mjumbe maalum wa Umoja wa Afrika na wapatanishi wenzake watatu wa kutoka jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi ya Afrika Magharibi-ECOWAS- wameondoka Abidjan bila ya kuzungumzia lolote lililofikiwa.

Waziri mkuu wa Kenya, Raila Odinga, ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP hivi punde, viongozi wote wawili wanaohasimiana nchini Côte d'Ivoire, Laurent Gbagbo na Alassane Outtara, wamekubali kukutana ana kwa ana, lakini kwa masharti maalum.

Hata hivyo mshauri wa masuala ya kidiplomasia wa Alassane Outtara, Ali Coulabaly, amekanusha habari hizo, huku Outtara akisema:

"Kwa upande wetu, mazungumzo yameshamalizika. Tumewaamabia wapatanishi wana mengi bado ya kufanya.Tunawashukuru kwa juhudi zao zote."

Wapatanishi wa ECOWAS na Umoja wa Afrika wameelekea Abuja ambako hivi punde wamekutana na mwenyekiti wa jumuia ya ECOWAS,rais Goodluck Jonathan wa Nigeria kumuarifu matokeo ya juhudi zao. Kiongozi huyo wa Nigeria aliahidi wiki iliyopita "hatua mpya" zitachukuliwa kuanzia leo.

Alassane Ouattara, mtu anayesemekana kuwa mshindi wa uchaguzi wa Rais, nchini Cote d'Ivoire

Alassane Ouattara, mtu anayesemekana kuwa mshindi wa uchaguzi wa Rais, nchini Cote d'Ivoire

Ili kusaidia kuumaliza mgogoro huo,serikali ya Marekani inasema iko tayari kumpokea Laurent Gbagbo pindi akiamua kuondoka kwa hiari madarakani.

Juhudi hizi za upatanishi mtu anaweza kusema ni shida kufanikiwa,seuze tena Laurent Gbagbo ameshasema hafikirii kulihama kasri la rais mjini Abidjan, licha ya shinikizo la kimataifa.

"Hatutokubali" aliahidi Gbagbo katika hotuba yake ya mwaka mpya, akikosoa kile alichokiita "njama ya mapinduzi inayoongozwa na jumuia ya kimataifa."

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP, REUTERS

Mpitiaji: Miraji Othman

 • Tarehe 04.01.2011
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/ztJk
 • Tarehe 04.01.2011
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/ztJk

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com