1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kupunguza mvutano kati ya Uturuki na Irak

Oummilkheir25 Oktoba 2007

Ujumbe wa ngazi ya juu wa irak watarajiwa kuwasili Ankara baadae leo

https://p.dw.com/p/C77W
Wanajeshi wa Uturuki waelekea katika mpaka na Irak
Wanajeshi wa Uturuki waelekea katika mpaka na IrakPicha: AP

Ujumbe wa ngazi ya juu wa Irak unatarajiwa kufika ziarani mjini Ankara leo jioni,baada ya uongozi wa Uturuki kuishauri serikali itangaze vikwazo vya kiuchumi ili kuitia kishindo Irak iache kushirikiana na waasi wa kikurd.

„Ujumbe wa watu sabaa unatazamiwa kuwasili saa kumi na moja za jioni leo“ mwanadiplomasia mmoja ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP.Hakutoa lakini maelezo zaidi.

Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Uturuki,ikihojiwa na shirika hilo la habari,imekwepa kuthibitisha au kukanusha habari hizo.

Mkutano wa ujumbe huo wa maafisa sabaa wa ngazi ya juu pamoja na wenzao wa Uturuki,umelengwa kuzuwia hujuma za jeshi la Uturuki dhidi ya vituo vya waasi wa chama cha wafanyakazi wa kikurd-PKK,kaskazini mwa Irak.

Mvutano kati ya Baghdad na Ankara umezidi makali baada ya waasi wa PKK kuwauwa wanajeshi 12 wa Uturuki jumapili iliyopita na kuwateka nyara wengineo wanane.

Ziara ya ujumbe wa Irak mjini Ankara inafuatia ziara ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uturuki Ali Babacan ,jumanne iliyopita mjini Baghdad.

„Ujumbe wa Irak,ikiwa kweli utakuja,utahitaji kua na mapendekezo madhubuti,la sivyo ziara yao haitakua na maana yoyote“ alionya mwanadiplomasia huyo wa Uturuki aliporejea nyumbani kutoka ziarani mjini Baghdad.

Ziara ya Ali Babacan mjini Baghdad ilipelekea serikali ya Baghdad kutangaza hatua za mwanzo dhidi ya harakati za waasi wa PKK´nchini Irak.Serikali ya Irak imepiga marufuku harakati za waasi wa PKK katika maeneo ya kaskazini na kuamuru zifungwe ofisi zote za chama hicho kinachotajwa na Marekani na nchi za Umoja wa ulaya kua ni miongoni mwa makundi ya kigaidi.

Hali ni tete katika eneo la kaskazini la Irak linalopakana na Uturuki.Madege ya kivita na helikopta za Uturuki zimehujumu vituo vya wakurd jana .Waasi 40 wa kikurd waliojipenyeza katika eneo hilo wametimuliwa na wanajeshi wa Uturuki.Waasi hao walilenga kuvishambulia vituo vya Gendarmerie katika mji wa milimani wa Hakkari.Mapigano makali yameripotiwa na watu kadhaa kuuliwa.

Marekani imeitaka Irak itekeleze ahadi ilizotoa za kuwachukulia hatua kali waasi wa PKK.Katibu wa dola katika wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani anaeshughulikia masuala ya ulaya Daniel Fried anasema:

„Pengine hatutaweza kutarajia kupata majib u ya mia bin mia,lakini tunahitaji kuona juhudi zikishika kasi mia bin mia.Na kuna mambo yanayoweza kutekelezwa hapo hapo na viongozi wa Irak,walioingiwa na hofu kuhusu mamlaka ya nchi yao,wanabidi wayatekeleze.”

Jana usiku baraza la usalama wa taifa la Uturuki limeitaka serikali ya Uturuki iyawekee vikwazo vya kiuchumi makundi yote wa wakurd wanaoshirikiana na waasi wa PKK,kaskazini mwa Irak.

Rais Abdullah Gul amesema hivi punde subira ya Uturuki imefikia kikomo,kila hatua itachukuliwa ili kuepukana na vitisho vinavyosababishwa na waasi wa PKK.

Wakati huo huo habari zinasema madege kadhaa ya kivita ya Uturuki chapa F-16 yameondoka Diyarbakir-mji wa kusini mashariki ya Uturuki wenye wakaazi wengi wa kabila la Kurd.