1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mwaka mmoja baada ya vita vya Gaza.

Abdu Said Mtullya23 Desemba 2009

Israel na Hamas wanafanya mazungumzo juu ya kubadilishana wafungwa mwaka mmoja baada ya vita vya Gaza.

https://p.dw.com/p/LCUg
Askari wa Israel wakitayarisha mashambulio.Picha: picture-alliance / dpa

Wiki hii unatimia mwaka mmoja tokea majeshi ya Israel yaiingie Gaza na kuwashambulia wapiganaji wa Hamas. Mashambulio hayo yaliyochukua wiki kadhaa yalimalizika tarehe 8 mwezi januari.

Lakini mashariki ya kati bado inaweza kulipuka tena wakati wote wote .

Vita vya Gaza mwaka mmoja uliopita vilikuwa vya mauaji makubwa.Vita hivyo vilianza tarehe 28 mwezi desemba mwaka jana na vilimalizika tarehe 8 mwezi januari.

Mashirika yanayotetea haki za binadamu yamesema wapalestina 1400 waliuawa katika vita hivyo, idadi kubwa walikuwa raia. Waisraeli 13 walikufa, askari pamoja na raia.

Vita vilianza baada ya wapiganaji wa kipalestina kuzishambulia sehemu za kusini mwa Israel kwa roketi na kadri vita vilivyokuwa vinaendelea ,vivyo ndivyo masafa ya roketi hizo yalivyokuwa yanazidi kuwa marefu.

Makombora hayo yalizifikia sehemu ambazo hapo awali hazikuwahi kuguswa.

Mashariki ya kati bado ni sehemu inayoweza kulipuka tena wakati wowote.

Jumuiya ya kimataifa inafanya juhudi za kuutatua mgogoro wa mashariki ya kati kwa njia ya mazungumzo.

Mjumbe wa Ujerumani kwa sasa yupo Gaza katika juhudi za kupatanisha katika mchakato wa kubadilishana wafungwa.

Mapema leo mpatanishi huyo alikabidhi pendekezo la Israel kwa Hamas juu ya msingi wa makubaliano ya kuachiwa kwa wafungwa wa kipalestina ikiwa Hamas itakuwa tayari kumwachia askari wa Israel Gilad Shalit alietekwa na wapiganaji wa kipalestina miaka mitatu na nusu iliyopita.

Kwa mujibu wa habari,kimsingi Israel ipo tayari kufikia mapatano lakini imesema haitaki baadhi ya wafungwa watakaoachiwa warudi kwenye Ukingo wa Magharibi.

Chini ya makubaliano yanayokusudiwa kutekelezwa Israel itawaachia wafungwa wapatao alfu moja wa kipalestina ikiwa Hamas itamwachia askari wa Israel- Gilad Shalit alietekwa miaka mitatu na nusu iliyopita.

Umoja wa Mataifa na nchi za magharibi zinatumai hatua ya kubadilishana wafungwa itachangia katika kuondoa kabali ya Israel iliyopo kwenye shingo ya Gaza.

Mwandishi/Mtullya Abdu.AFPE/ZA

Mhariri/Othman, Miraji