1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za amani nchini Syria

10 Julai 2012

Mjumbe wa kimataifa anaesaka ufumbuzi wa mzozo wa Syria,Kofi Annan, yuko ziarani mjini Teheran ambako amepanga kuzungumza na viongozi wa serikali ya Iran -washirika wakubwa wa Syria.

https://p.dw.com/p/15Ub0
Mjumbe wa kimataifa Kofi Annan akizungumza na waandishi habariPicha: Reuters

Ziara ya mjumbe huyo maalumu wa Umoja wa mataifa na jumuiya ya nchi za kiarabu nchini Iran inafanyika siku moja baada ya mazungumzo Kofi Annan aliyokuwa nayo jana mjini Damascus pamoja na rais wa Syria, Bashar al Assad, ambapo walikubaliana kuhusu "utaratibu mpya" wa kuumaliza mzozo wa karibu miezi 16 ambao tayari umeshaangamiza maisha ya zaidi ya watu 17 elfu.

"Iran inabidi iwe sehemu ya ufumbuzi wa mzozo wa Syria" amesema mjumbe huyo maalumu wa Umoja wa mataifa baada ya mazungumzo pamoja na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran, Ali Akbar Salehi, mjini Teheran.

Kabla ya hapo Kofi Annan alisema:"Kama mjuavyo tume ya mkakati ilikutana mwishoni mwa mwezi Juni mjini Geneva kwa hivyo nimekuja kuzungumzia matokeo ya mazungumzo hayo na kuona jinsi tutakavyoweza kushirikiana na kusaidia kurekebisha hali ya mambo nchini Syria."

Kwa mujibu wa duru za Umoja wa Mataifa, Kofi Annan anaamini mchango wa Iran ni muhimu katika kuumaliza mzozo wa Syria na kwamba Iran inaweza kutumia ushawishi wake kufikia makubaliano ya kumaliza matumizi ya nguvu.

Libanon Syrien Artilleriebeschuss
Nyumba moja yashambuliwa na vikosi vya Syria huko Wadi Khaled kaskazini mwa LibnanPicha: Reuters

Serikali ya Iran imesema kwa mara nyengine tena inaunga mkono kikamilifu mpango wa amani wa Kofi Annan. Katika mkutano na waandishi habari pamoja na mjumbe huyo wa kimataifa, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran, Ali Akbar Salehi, amesema wanataraji ufumbuzi utapatikana ili kuepukana na kitisho cha mzozo wa Syria kuenea katika eneo hilo.

Mapigano yalipamba moto jana usiku nchini Libnan. Mizinga iliyofyetuliwa kutoka Syria imepiga katika ardhi ya Libnan kufuatia mapigano kwa mtutu wa bunduki kutoka pande zote mbili za mpakani.

Kutokana na hali hiyo mkuu wa baraza la taifa la Syria, muungano wa upande wa upinzani, Abdel Basset Sayda, ameitolea mwito Urusi iache kuipatia silaha serikali ya Damascus. Sayda amesema atalizungumzia suala hilo atakapokutana na viongozi wa Urusi kesho mjini Moscow. Wakati huo huo, Urusi imesema haitotiliana saini makubaliano mapya ya silaha na Syria, ikiwa hali haijarejea kuwa ya kawaida nchini humo.

Genf Syrien Konferenz Kofi Annan
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Urusi Serguei Lavrov na mjumbe wa kimataifa Kofi Annan(kulia).Picha: dapd

Serikali ya Urusi imesema hii leo inataka kuitisha mkutano mwengine wa madola ya kigeni kuhusu mzozo wa Syria. Imesisitiza hata hivyo mkutano huo haustahiki kuzungumzia hatima ya rais Bashar al Assad.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa/Reuters/AFP

Mhariri:Josephat Charo