1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Johnson ajitowa kinyang'anyiro cha uwaziri mkuu Uingereza

30 Juni 2016

Kinyan'ganyiro cha kuwania nafasi ya waziri mkuu mpya wa Uingereza kimechukuwa sura mpya baada ya meya wa zamani wa mji wa London Boris Johnson kung'atuka kwa ghafla katika kinyang'anyiro hicho.

https://p.dw.com/p/1JGtL
Picha: Reuters/T. Melville

Boris Johnson ambaye alikuwa mpiga debe mkuu katika kampeni ya kutaka Uingereza ijitowe katika Umoja wa Ulaya ameuambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba kiongozi mpya wa chama tawala cha Kihafidhina atatakiwa kukiunganisha chama hicho na kuhakikisha Uingereza inasimama kwa fahari duniani.

Johnson amesema "Baada ya kushauriana na wenzangu na kuzingatia mazingira yaliyoko bungeni nimeamuwa kwamba mtu huyo hawezi kuwa mimi.Kazi yangu itakuwa kutowa msaada kadri inayowezekana kwa utawala mpya wa kihafidhina kuhakikisha tunatimiza kikamilifu matakwa ya wananchi ambayo yamewasilishwa katika kura ya maoni na kupigania agenda ninayoiamini."

Johnson amejitowa katika kinyan'ganyiro hicho baada ya waziri wa sheria na mshirika wake mkuu Michael Gove kuacha ghafla kumuunga mkono na kutangaza kwamba yeye mwenyewe binafsi anawania wadhifa huo wa kukiongoza chama cha kihafidhina na kushika wadhifa wa waziri mkuu mpya wa Uingereza.

Matunda aliyovuna Johnson

Uamuzi wa Johnson mwenye umri wa miaka 52 kuvunja uhusiano na mshirika wake wa muda mrefu Cameron na kuunga mkono kambi inayotaka kujitowa kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya imezaa matunda wiki iliopita wakati Cameron alipojiuzulu baada ya wapiga kura kuamuwa katika kura ya maoni kujitowa katika Umoja wa Ulaya kwa asilimia 52 dhidi ya 48.

Waziri wa sheria Michael Gove na mke wake Sarah Vine.
Waziri wa sheria Michael Gove na mke wake Sarah Vine.Picha: Getty Images/J. Taylor

Waziri wa mambo ya ndani Theresa May,waziri wa ujenzi na kazi Stephen Crabb,waziri wa nishati Andrea Leadson na waziri wa zamani wa ulinzi Liam Fox pia wamo katika kinyan'ganyiro hicho.

Mshindi atakayetangazwa Septemba tisa atakuwa waziri mkuu na kuwa na dhima muhimu ya kujenga aina ya uhusiano itakaokuwa nao Uingereza na Umoja wa Ulaya.

Donda la kujitakia

Gove ambaye amefanya kampeni ya pamoja kuienguwa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya amesema katika taarifa kwamba amefikia uamuzi huo shingo upande kwamba Boris hawezi kuwasilisha uongozi au kujenga timu kukabiliana na kazi ilioko usoni na kwa hiyo ameamuwa kuliwasilisha jina lake kuwania uongozi huo.

Theresa May waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza.
Theresa May waziri wa mambo ya ndani wa Uingereza.Picha: Getty Images/C. Court

John MCFarlane mwenyekiti wa kampuni ya TheCityUK ambayo inaendeleza sekta ya kifedha ya Uingereza ametowa wito wa kuwepo kwa uongozi imara na unaofaa wa kisiasa pamoja na ufasaha wa kile inachokitaka Uingereza katika mazungumzo yake na Umoja wa Ulaya kutibu jeraha la kujitakia.

McFarlane ambaye pia ni mwenyekiti wa benki ya Barclays amesema aidha hawajuwi umbo wala mwelekeo wa jinsi mambo yatakvyokuwa huko mbele.

Ameuambia mkutano wa kila mwaka TheCityUK kwamba "bado haifahamiki kabisa kile ambacho yumkini tunaweza kukipata kutoka katika mazungumzo hayo na Umoja wa Ulaya."

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AP/dpa

Mhariri : Josephat Charo