1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Joe Biden kuteuwa baraza lake la kwanza la mawaziri

Saumu Mwasimba
23 Novemba 2020

Rais mteule Joe Biden anatarajiwa kumteuwa Antony Blinken kuwa waziri wa mambo ya nje katika baraza lake la mawaziri. Na wakati huohuo mipango ya maandalizi ya shughuli ya kumuapisha rais, Januari 20 inaendelea.

https://p.dw.com/p/3lika
USA I Wahlen I Biden in Georgia
Picha: Drew Angerer/Getty Images

Washauri wa rais mteule Joe Biden wamefahamisha kwamba watatangaza orodha ya kwanza ya baraza la mawaziri kesho Jumanne. Ingawa pia inatajwa kwamba maseneta wa chama cha Democratic wanafikiriwa kupewa nafasi za kiserikali na chama hicho kinatarajia kurudisha ushindi wa baraza la seneti.

Ikumbukwe kwamba udhibiti wa baraza hilo bado haujulikani hatma yake huku matokeo ya chaguzi mbili za marudio katika jimbo la Gergia zikisubiriwa mwezi Januari ambapo kwahakika matokeo hayo ndiyo yatatowa mwelekeo kamili wa nani wa kulidhibiti baraza hilo la Seneti la Marekani.

Antony Blinken mwenye umri wa miaka 58 anatajwa katika uwaziri wa mambo ya nje

Deutschland Berlin US Vizeaußenminister Antony Blinken
Mwanasiasa Antony BlinkenPicha: picture alliance/AA/A. Simsek

Hivi sasa macho ya Wamarekani na jumuiya ya kimataifa yanasubiri kuona nani watateuliwa katika baraza la mawaziri la Marekani. Imeshadokezwa na duru za watu wa karibu na timu ya mipango ya Biden kwamba Antony Blinken mwenye umri wa miaka 58 ndiye atakayeteuliwa katika nafasi ya waziri wa mambo ya nje.

Ifahamike kwamba Blinken aliwahi kuwa naibu waziri wa mambo ya nje na pia naibu mshauri wa masuala ya usalama wa taifa chini ya uongozi wa serikali ya Barack Obama,na ni mtu aliyeko karibu na rais mteule Joe Biden.

Ikiwa Blinken atateuliwa na kuthibitishwa katika nafasi hiyo basi atakuwa mtu aliyeko kwenye nafasi ya juu katika serikali ijayo na hasa katika kuupangua na kuujenga upya uhusiano wa Marekani na nchi nyingine za ulimwengu baada ya miaka minne ya rais Donald Trump ambaye serikali yake imekuwa ikihoji kuhusu ushirikiano wa muda mrefu na washirika wa nchi hiyo.

Lakini pia ikiwa Biden atamteua Blinken atafanikiwa kuepuka uwezekano wa kuibuka masuala tete ambayo yangeweza kusababisha athari ya kutoidhinishwa na baraza la Seneti, endapo atawateua wagombea wengine wawili waliorodheshwa kuwa na uwezekano wa kupewa wadhifa huo,Susan Rice na Seneta Chris Coons.

Utata wa kumteuwa mwanasiasa mkongwe Susan Rice

USA Nationale Sicherheitsberaterin Susan Rice
Mwanasiasa mkongwe wa Marekani Susan RicePicha: Reuters/J. Roberts

Endapo angemteua Susan Rice inaelezwa kwamba angekabiliwa na upinzani mkubwa na pengine kukataliwa kwenye Seneti kwasababu ni mtu ambaye amekuwa akilengwa kwa muda mrefu na Republicans kutokana na kauli zake alizowahi kutowa baada ya mashambulizi ya mwaka 2012 dhidi ya Wamarekani katika mji wa Beghazi nchini Libya.

Joe Biden pia huenda akaliteua baraza lake la mawaziri kwa awamu ambapo awamu ya mwanzo itakayotangazwa mara moja inaweza kujikita katika masuala maalum,kama uchumi,usalama wa ndani,na Afya.

Juu ya hayo Ron Klain mkuu wa shughuli za ofisi ya rais ajaye Joe Biden jana alisema serikali ya Trump inakataa kuwasafishia njia ya kuanza kupata taarfa muhimu kuhusu mashirika na taasisi muhimu za nchi kwa ajili ya shughuli ya kukabidhi madaraka na hatua hiyo inaathiri mipango hiyo ikiwemo mchakato huo wa kuteua baraza la mawaziri.

Soma zaidi:Biden asema hataifunga nchi licha ya maambukizi kuongezeka

Pamoja na yote hayo kinachosubiriwa ni baraza jipya la mawaziri nchini Marekani na nchi kama Ujerumani,Ufaransa na Uingereza mawaziri wao wa mambo ya nje wanakutana leo kujadili hatma ya makubaliano ya kimataifa ya Nuklia ya Iran huku yakiwepo matumaini kwamba serikali mpya ya Marekani huenda ikasaidia kuleta uhai mpya katika makubaliano hayo.

Chanzo:AP