Jirga ya Afghanistan yakutana kuijadili Marekani | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.11.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Jirga ya Afghanistan yakutana kuijadili Marekani

Baraza la Wazee wa Afghanistan, Loya Jirga, linakutana leo (16.11.2011)mjini Kabul huku Rais Hamid Karzai akitoa masharti mapya kwa majeshi ya Marekani kuendelea kubakia nchini mwake na Taliban wakiapa kushambulia.

Rais Hamid Karzai wa Afghanistan akifungua mkutano wa Loya Jirga, tarehe 16.11.2011 mjini Kabul.

Rais Hamid Karzai wa Afghanistan akifungua mkutano wa Loya Jirga, tarehe 16.11.2011 mjini Kabul.

Akizungumza kwenye ufunguzi wa baraza hilo, Rais Hamid Karzai amesema ushirikiano wa Afghanistan na Marekani, lazima uzingatie kumalizika mara moja kwa mashambulizi ya nyakati za usiku yanayofanywa na NATO na pia jeshi la kimataifa kuvikabidhi vikosi vya usalama vya Afghanistan jukumu la ulinzi na udhibiti wa mahabusu.

"Tunataka kuwa na mashirikiano imara na Marekani na NATO, lakini kwa masharti. Tunataka uhuru wa mamlaka yetu na kumalizika kwa mashambulizi ya usiku na kukamatwa kwa watu wetu. Hatutaki pawepo na mfumo mwengine kando ya serikali yetu." Amesema Karzai.

Baraza la Jirga lenye wajumbe 2,000 linawashirikisha viongozi wa makabila mbalimbali katika nchi hiyo ambayo utiifu kwa makabila ni jambo la msingi. Mkutano wa leo unajadili masharti ya kuendelea kuwapo kwa wanajeshi wa Marekani ndani ya nchi yao katika miaka ijayo na pia uwezekano wa mazungumzo na Taliban.

Kwa mujibu wa watu wenye uelewa na mijadala hii, masharti ya Karzai yamekuwa hayakubaliki na Marekani, ingawa maafisa wa serikali ya Marekani, wamesema wanaliunga mkono Jirga. Karzai amedokeza pia kuwa serikali yake inafanya kazi ya kuwa na mashirikiano na Ufaransa, Uingereza, Australia na Umoja wa Ulaya.

Wabunge walipinga Jirga

Baadhi ya wajumbe wa mkutano wa Loya Jirga wakiingia ukumbini tarehe 16.11.2011 mjini Kabul.

Baadhi ya wajumbe wa mkutano wa Loya Jirga wakiingia ukumbini tarehe 16.11.2011 mjini Kabul.

Kisheria, Jirga halina nguvu, lakini kama litaridhia matakwa ya Karzai, litakuwa limempa uzito wa kisiasa kufanya makubaliano juu ya mpango wa kubakisha baadhi ya vikosi vya Marekani nchini Afghanistan kwa muongo mwengine, licha ya upinzani mkali.

Wabunge wa Afghanistan wameuita mkutano huu wa Jirga kuwa kinyume na katiba, kwa kuwa unalitenga Bunge ambalo ni chombo cha kujadili na kupitisha maamuzi ya kitaifa kama hili.

Wabunge wanamtuhumu Karzai kulitumia Jirga kwa manufaa yake ya kisiasa, ikiwemo kutafuta uungwaji mkono wa kugombea uraisi kwa mara ya tatu. Lakini Karzai mwenyewe amesema baraza hilo ni kwa ajili ya mashauriano tu, na sio kufanya maamuzi.

Kwa upande wao, Taliban wameupinga mkutano huu wa leo, wakiuita "jaribio la Marekani kuhalalisha kuwapo kwa majeshi yake nchini Afghanistan". Kundi hilo limeapa kufanya mashambulizi ya kuuchafua mkutano huo.

Hali ya usalama imeimarishwa mjini Kabul kufuatia kitisho hicho. Polisi na maafisa wa usalama wa taifa wamesambazwa maeneo kadhaa ya mji huo. Vizuizi vimewekwa barabarani na kuzunguka ukumbi wa mkutano.

Katika mkutano kama huu mwaka jana, Taliban waliliwasha moto hema la mkutano, tukio lililouchafua mkutano wenyewe ingawa halikusababisha maafa yoyote. Mashambulizi hayo ya mwaka jana yalisababisha kujengwa kwa jengo imara zaidi, ambalo haliwezi kuathiriwa na moto.

Huku mkutano huo ukiendelea, NATO imesema maafisa wake watatu wameuawa kusini mwa Afghanistan, baada ya kushambuliwa. Taarifa ya NATO haikutaja undani wa tukio lenyewe, lakini kiasi ya wanajeshi 14 wa kimataifa wameshauawa nchini Afghanistan kwa kipindi cha wiki mbili zilizopita, na wanamgambo wa Taliban.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

 • Tarehe 16.11.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/13BXs
 • Tarehe 16.11.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/13BXs

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com