Jihadi ni sasa, waonya Waislamu nchini Somalia. | Habari za Ulimwengu | DW | 23.10.2006
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

Jihadi ni sasa, waonya Waislamu nchini Somalia.

Viongozi wa mahakama za kiislamu nchini Somalia, wametishia kuanza vita vya jihadi dhidi ya wanajeshi wa Ethiopia wanaodaiwa wapo nchini humo.

Raia wa Somalia wajiandaa kwa vita.

Raia wa Somalia wajiandaa kwa vita.

Serikali ya Ethiopia nayo ikijibu wito huo wa kiongozi wa mahakama za kiislamu Sheikh Hassan Dahir, ilisema iko tayari kwa lolote.

Katika hotuba kali mwishoni mwa mwezi mtukufu wa Ramadhan, Sheikh Dahir aliwataka raia wote wa Somalia kusimama imara na kuilinda nchi yao.

Kiongozi huyo wa kidini amesema muda wa kuwataka Waethiopia kuondoka katika ardhi ya Somalia umekwisha na kilochobaki sasa ni kuchukua hatua za kivita, dhidi ya wavamizi wa kiethiopia.

Akitoa hotuba hiyo katika msikiti mmja mjini Mogadishu, Sheikh Dahir amewataka Waethiopia kuondoka kabla mambo hayajaharibika……la sivyo watakiona chamtema kuni….kwani maiti zao zitatapakaa katika ardhi ya Somalia.

Kiongozi huyo pia ameongeza kusema hawatothubutu tena kuuambia ulimwengu kwamba Ethiopia inaingilia kati maswala ya Somalia.

Alisema na hapa tunamnukulu….” Sasa tutaanza vita, ninawataka raia wote wa Somalia popone walipo kuanza vita vya jihadi dhidi ya wavamizi na wale wanaowaunga mkono wavamizi hao.

Matamshi hayo ya Aweis yameonekana kuzilenga serikali hafifu ya mpito ya Somalia na ile ya Addis Ababa, ambapo kwa pamoja zimekuwa zikikanusha kuwepo kwa wanajeshi wa Ethiopia katika ardhi ya Somalia.

Licha serikali ya Ethiopia kuapa kujilinda na kuilinda serikali ya mpito ya rais Abdillahi Yusuuf dhidi ya wanamgambo wa kiislamu imekiri kuwapeleka wakufunzi wa kijeshi huko Somalia, lakini ni idadi ndogo tu, na wala si maelfu kima inavyodaiwa na wafuasi wa Sheikh Dahir.

Pamoja na hilo Ethiopia imeonya kwamba itaangilia kati endapo wanamgambo hao wa kiislamu wataivamia serikali ya mpito kufuatia mgogoro uliopo juu ya mji wa Burhakaba uliokaribu na makao makuu ya muda ya serikali ya mpito, huko Baidoa.

Inaaminika kwamba mwishoni mwa wiki, wapiganaji waliokuwa na silaha walikusanyika karibu na mji huo wa Burhakaba baada ya washirika wao kutimuliwa na wanajeshi wa serikali ya mpito katika eneo hilo.

Kwa muujibu wa mkuu wa usalama wa kundi hilo la kiislamu, Sheikh Yusuf Mohammed Siyad, wapiganaji wake wameuchukua tena mji huo, na kwa sasa uko chini ya udhibiti wa viongozi hao wa kiislamu.

Wadadisi na wanadiplomasia wanahofia huenda mgogoro kati ya serikali ya mpito na wanamgambo wa kiislamu kuikarudisha eneo hilo la upembe wa Africa katika mapigano.

Na hilo litasababisha kuwapa nguvu wapiganaji wa kiislamu na hasa ikiwa Ethiopia itaaingilia moja kwa moja mgogoro huo, na huenda ukaingiza kati nchi jirani ya Eritrea inayodaiwa kuwaunga mkono wapiganaji wa Kiislamu.

 • Tarehe 23.10.2006
 • Mwandishi Munira Muhammad
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CBI7
 • Tarehe 23.10.2006
 • Mwandishi Munira Muhammad
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CBI7

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com