1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jibu la waziri mkuu wa Israel kwa pendekezo la nchi za Kiarabu.

2 Aprili 2007

Katika mwenendo wa amani wa Mashariki ya kati yaonesha tena kuna mambo yanayotendeka. Wiki iliopita, Umoja wa Nchi za Kiarabu, Arab League, uliupendekeza tena ule mpango wa amani uliotolewa na Saudi Arabia ambao unakubali kuitambua kamili Israel pindi dola hiyo ya Kiyahudi itarejea nyuma katika mipaka iliokuweko mwaka 1967 baina yake na nchi za Kiarabu.

https://p.dw.com/p/CB4w
Waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert.
Waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert.Picha: AP

Jibu la kimapinduzi lilitolewa kwa mara ya kwanza jana na waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, alipokutana na rais wa Umoja wa Ulaya, Kansela wa Ujerumani, Bibi Angela Merkel. Bwana Olmert yeye alizialika nchi zote za Kiarabu, ikiwa pamoja na Wapalastina, katika mkutano wa kilele.

Mambo hayajawa mazuri kwa waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert. Kwanza malalamiko makubwa anayokabiliana nayo miongoni mwa watu wa nchi yake kutokana na kushindwa vita alivoendesha huko Libanon katika majira ya kiangazi ya mwaka jana dhidi ya wanamgambo wa Hizbullah. Tena kumefuata muungano baina ya vyama vya Hamas na Fatah na kuundwa serekali ya Umoja wa Taifa ya Wapalastina, jambo ambalo lililopelekea kudhoofika ule upinzani wa nchi za Magharibi dhidi ya serekali iliokuwa inaongozwa na Chama cha Hamas. Na sasa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Arab League, katika mkutano wake huko Riyadh, Saudi Arabia, umekariri tena pendekezo lake la kutaka kuwa na amani na Israel. Sharti iliotoa ni kwamba dola hiyo ya Kiyahudi iwe tayari kuziwachia ardhi ilizoziteka na iwaruhusu wakimbizi wa Kipalastina warejee makwao. Pale mpango huo ulipopendekezwa mwanzo miaka mitano iliopita, Israel iliukataa, ikidai masharti yake hayakubaliki. Leo, lakini, Ehud Olmert hawezi kutoa jibu kama hilo. Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, aliweka wazi kuhusu jambo hilo hata kabla ya mkutano wa Riyadh, na bila ya shaka waziri mkuu wa Israel aligundua hisia zilivyo katika mawasiliano yake na nchi za Ulaya. Kwanini jibu hili la Israel litolewe wakati wa ziara ya karibuni ya Kansela wa Ujerumani huko Israel? Pale Ehud Olmert anaposema yuko tayari kuwa na mkutano wa amani na viongozi wa Kiarabu, basi hiyo sio kuwa anakusudia kweli kweli kuelekea kwenye amani ya Mashariki ya Kati, anajitoa tu kimasomaso. Kwani mkuu huyo wa serekali ya Israel ameongeza kusema kwamba yeye bila ya shaka atafanya mazungumzo wa Kiarabu wenye siasa za wastani, na kwamba bado Israel ina ati ati kuhusu pendekezo hilo la kutoka Riyadh.

Kwa hakika bado Israel inakataa kuziwachia ardhi zote za Waarabu ilizoziteka katika vita vya mwaka 1967, na hasa haitaki kuiwachia sehemeu ya mashariki ya Jiji la Jerusalem ilioiunganishwa na nchi yake. Pia inakataa kuwapa haki ya kurejea makwao katika ardhi ya sasa ya Israel wakimbizi wa Kipalastina waliohama kwa lazima mwaka 1948. Na kuhusu Israel kurejea katika mipaka ya mwaka 1967, msimamo wa Israel unapingana na ile fikra ya kimataifa, kwamba dola ya Kipalastina itakayoundwa iwemo katika zile ardhi zilizotekwa katika vita vya siku sita vya mwaka 1967 baina ya Israel na Waarabu. Kuhusu Israel kuwakatalia Wapalastina haki ya kurejea makwao, mtu anaweza kutazamia kwamba pale dola ya Kipalastina itakapokuweko pembeni na Israel, basi dola hiyo itawachukuwa wakimbizi hao wa mwaka 1948.

Lakini Jumuiya ya Nchi za Kiarabu haitakubali kuweko tafauti hiyo. Kwa upande wake pendekezo iliolitoa kwa Israel ni la kimapinduzi tosha na haiko tayari kupatana na Israel kuhusu jambo hilo. Ndio maana jibu hilo la Ehud Olmert ni maneno matupu. Mkutano huo wa amani anaofikiria yeye hautaweza kamwe kuweko. Yeye mwenyewe waziri mkuu huyo wa Israel anatambua hivyo, ama sivyo asingesema kwamba anataka kuzungumza tu na viongozi wa Kiarabu walio na msimamo wa wastani.

Bila ya shaka, hiyo ni sababu wazi ya kushindwa jambo hilo. Kama ilivyo, kimsingi, katika mizozo yote, Israel katika mzozo huu lazima iwe tayari kuzungumza na wapinzani wake walio na siasa kali. Kuwapata walio na siasa za wastani kuzungumza nao sio kazi ya usanii. Na hao walio na siasa kali hawataki kufanya mazungumzo na Israel kwa msingi huo iliojiwekea Israel. Kwa hivyo ni wazi, hakutakuweko na jambo, juhudi hizo zitashindwa tu.

Miraji Othman