1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jeshi Nigeria katika vitisho vipya vya Boko Haram

8 Septemba 2016

Jeshi la Nigeria limekomboa maeneo makubwa kutoka kwa Boko Haram, lakini vitisho vya uvamizi wa kuvizia vinaonyesha namna gani hali bado ni tete kaskazini-mashariki mwa Nigeria baada ya uasi wa kikatili wa kundi hilo.

https://p.dw.com/p/1JycF
Kiongozi wa kikosi cha kanda kinachopambana dhidi ya Boko Haram, Meja Jenerali Iliya Abbah (kulia) akizungumza sambamba na matangulizi wake ambaye ndiye mkuu wa majeshi ya Nigeria Jenerali Tukur Buratai.
Kiongozi wa kikosi cha kanda kinachopambana dhidi ya Boko Haram, Meja Jenerali Iliya Abbah (kulia) akizungumza sambamba na matangulizi wake ambaye ndiye mkuu wa majeshi ya Nigeria Jenerali Tukur Buratai.Picha: Getty Images/AFP

Mara baada ya misafara ya magari ya kijeshi kuondoka katika mazingira salaama ya Bama - mji wa pili katika jimbo la Borno wanajeshi walioko kwenye gari la mbele hufyatua sihala nzito nzito kwenye magugu yalioko pembezoni mwa barabara ili kuzuwia mashambulizi ya kuvizia kutoka kwa masalia wa wapiganaji kutoka kundi hilo la itikadi kali.

Wakati wakielekea kwenye mji mkuu wa jimbo Maiduguri, wanajeshi hao wanakagua barabara kuona kama kuna mabomu na mitego, huku wakifyatua risasi dhidi ya chochote kinachoonekana kuwa kitisho -kama vile kwenye vituo vya mafuta vilivyotelekezwa, majumba ya mashambani yaliochoma moto, miti na hata vichaka vya majani ya tembo.

Madereva wa magari wanaowafuata kwa nyuma nao wanajiunga katika kufyatua hovyo silaha za mashambulizi kupitia vioo vya magari kwa kutumia mkono mmoja huku mkono mwingine ukibakia usukani. Ikiwa kuna mtu huko na unamfyatulia risasi basi naye atataka kurudisha mashambulizi, hivyo unajua alipo na kuchukuwa hatua," anasema Kanali Adamu Laka, kamanda wa kijeshi mjini Bama.

Hatua za tahadhari kubwa kama hizo zinamulika hali ya ukosefu wa usalama katika jimbo la Borno licha ya mafanikio ya jeshi katika kulifurusha kundi la Boko Haram kutoka eneo lililokuwa likilidhibiti, ambalo miezi 18 iliyopita lilikuwa na ukubwa sawa na nchi ya Ubelgji.

Nigeria Soldaten in Damboa
Baadhi ya wanajeshi wa NIgeria wanaopambana dhidi ya Boko HaramPicha: Getty Images/AFP/S. Heunis

Makundi madogomadogo ya waasi

Shirika la habarila reuters lilialikwa na jeshi la Nigeria wakati likijaribu kurejesha utengamano jimboni Borno baada ya miaka saba ya udhibiti wa Boko Haram - mmoja ya makundi ya kikatili zaidi ya Kiislamu duniani, na changamoto kubwa serikali ambayo pia inakabiliana na mgogoro wa kiuchumi uliyosababishwa na kuporomoka kwa bei za mafuta.

Kama timu ya kwanza ya maripota wa kimataifa kusafiri katika eneo hilo kwa kutumia barabara tangu Boko Harama ilipoondoshwa, reuters ilijionea uharibifu uliyosababishwa na kundi hilo. Barabara zinakabaliwa na hatari kubwa, hakuna chakula kinacholimwa mashambani, na watu bado wanaendelea kujitokeza kutoka maficho yao vichakani.

Kampeni ya kijeshi imedhibiti uasi huo uliyogharimu maisha ya watu wasiopungua 15,000 tangu mwaka 2009 lakini katika awamu nyingine ya mgogoro huo, jeshi hilosasa linajikuta likipambana na makundi madogo madogo ya waasi yanayoendesha harakati zao katika maeneo ya misitu yasio na watu wengi.

Mwezi Julai wapiganaji wa Boko Haram waliojificha kwenye miti pembeni mwa barabara ya kutoka Bama kwenda Maiduguri waliuvamia msafara wa shirila la misaada la Umoja wa Mataifa na kuwajeruhi watu watano.

Wakati Umoja wa Mataifa unasema hadi watu milioni 5.5 kusini-mashariki mwa Nigeria huenda wakahitaji msaada wa chakula mwaka huu, jeshi linakabiliwa na shinikizo kubwa kuweka usalama barabarani. Hii siyo kazi rahisi. Kuna vituo kadhaa vya mashambulizi ya kuvizia hivyo tunakata miti," alisema Kanali Laka.

Nigeria Abuja Präsident Muhammadu Buhari
Rais wa Nigeria Muhammadu BuhariPicha: picture-alliance/dpa/W. Krumm

Changamoto ya huduma za msingi

Baada ya Boko Haram kufurushwa, serikali na mashirika ya misaada yameweza kutathmini kwa mara ya kwanza, ukubwa na janga la kibinaadamu lililoachwa na wapiganaji hao wanaojiita wa jihadi. Shirika la watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF, lilisema mwezi uliyopita kuwa karibu watoto nusu milioni wakao hatarini kukumbw ana utapiamlo katika eneo linalozunguka ziwa Chad, ambalo limeharibiwa na Boko Haram.

Kwa mujibu wa UNICEF, katika jimbo la Borno ambako vituo viwili kati ya vitatu vya afya vilihabriwa kwa sehemu au kabisaa, watoto 49,000 watakufa mwaka huu ikiwa msaada hautawasili. UNICEF ilisema vijiji na miji vimeharibiwa na jamii hazipati huduma za msingi.

Tangu Rais Muhammadu Buhari, kiongozi wazamani wa kijeshi alipochukuwa madaraka mwaka uliyopita, jeshi limepata motisha mpya dhidi ya Boko Haram, ambayo imekuwa ikipambana kuunda taifa linalofuata mfumo wa zamani wa Khilafa katika sehemu ya kusini mwa janagwa la Sahara.

Jeshi limehamishia makao yake mjini Maiduguri, kuajiiri majenerali wapya na kuboresha ushirikiano na nchi jirani, hivyo kuliwezesha kuteka na kudhibiti miji kadhaa kama vile Bama. Lakini masaibu ya Bama yanaonyesha ukubwa wa chamgamoto ya kulifufua eneo hilo kutokana na kampeni mbaya ya Boko Haram, ya kuchoma kila kitu katika meneo lilikopita.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre

Mhariri: Saumu Yusuf